1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabalozi wa Umoja wa Ulaya wahudhuria sherehe za kuapishwa Ahmadinejad.

Abdu Said Mtullya6 Agosti 2009

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wasema ni jambo la kashfa kushiriki kwa Umoja wa Ulaya kwenye sherehe za kuapishwa Ahmadinejad.

https://p.dw.com/p/J4eQ
Rais Mahmoud Ahmadinejad ameapishwa kutumikia kipindi cha pili, mabalozi ya Umoja wa Ulaya walihudhuria sherehe za kuapishwa kwake .Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya kuapishwa kwa rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran na juu ya kuachiwa kwa waandishi habari wa Marekani nchini Korea ya kaskazini.


Rais Mahmoud Ahmadinejad jana aliapishwa rasmi kutumikia kipindi cha pili cha urais nchini Iran kufuatia matokeo ya uchaguzi yaliyokuwa ya utatanishi.Miongoni mwa waalikwa kwenye sherehe hizo walikuwa mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya. Juu ya hayo mhariri wa gazeti la Oldenburgische anasema ni kashfa kwa mabalozi hao kushiriki katika sherehe hizo.

Gazeti hilo linasema hatua hiyo maana yake ni kusalimu amri mbele ya utawala ambao hapo awali ulishutumiwa na nchi za Umoja wa Ulaya.Mhariri huyo anaeleza kuwa hayo yanatokana na nchi hizo kuitegemea Iran kwa mahitaji ya gesi. Gazeti linasema hatua ya mabalozi hao imesababisha madhara makubwa.Umoja wa Ulaya umepoteza uadilifu wake duniani juu ya suala la kutetea haki za binadamu.

Na gazeti la Westfälische Nachrichten linaongeza kwa kusema kwamba wakati polisi wanawapiga virungu waandamanaji barabarani, rais Ahmadinejad anashangaliwa, na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya wanahudhuria sherehe za kuapishwa kwake.

Mhariri wa gazeti hilo anasema sababu iliyotolewa ni kwamba pana haja ya kudumisha mawasiliano ya kidiplomasia.Mhariri huyo anasema hayo yote ni sahihi, ili kuendeleza mazungumzo na Iran, lakini anahoji kwamba ingekuwa bora kwa Umoja wa Ulaya kujiweka mbali na sherehe hizo ili kutoa ishara dhahiri kwa watawala wa Iran.

Magazeti ya Ujerumani leo pia yanazungumzia juu ya kuachiwa huru jana kwa waandishi habari wa Marekani nchini Korea ya Kaskazini.

Gazeti la Aachener Nachrichten linasema sasa ni upuuzi kusema kwamba ,kwa kuenda Korea ya Kaskazini, aliekuwa rais wa Marekani Bill Clinton,hakuwa mbali sana na kuzungumza na magaidi.

Gazeti hilo linakumbusha kuwa ni kutokana na mazungumzo kwamba kuta la Berlin liliangushwa.

Na mhariri wa gazeti la Allgemeine Zeitung anaunga mkono hoja hiyo kwa kusema kwamba siasa ya mabavu ya rais Bush haikuleta manufaa katika suala la Korea ya Kaskazini.Gazeti linaeleza kuwa mafanikio ya siasa ya rais Obama yamethibitika katika kuachiwa kwa waandishi habari.

Hatahivyo gazeti la Reutlinger halikubaliani na hoja hizo. Gazeti hilo linasema ni jambo lisilokubalika kwa jumuiya ya kimataifa ,kufanya mazungumzo na utawala unaomiliki silaha za nyuklia na unaongozwa na kiongozi mgonjwa na kigeugeu.

Mwandishi/Abdul Mtullya.

Mhariri:M.Abdul-Rahman..