1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri.

Abdu Said Mtullya26 Aprili 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu waziri mteule anayetaka kupigwa marufuku kwa misalaba mashuleni.

https://p.dw.com/p/N78p
Waziri mteule Aygül ÖzkanPicha: AP

Magazeti ya Ujerumani leo yanazingatia kauli iliyotolewa na waziri mteule wa jimbo la Lower Saxony aliesema kwamba misalaba pia inapaswa kupigwa marufuku mashuleni nchini Ujerumani.Magazeti hayo pia yanazungumzia juu ya mgogoro wa madeni unaoikabili Ugiriki.

Waziri mteule Aygül Özkan anaetarajiwa kuishika wizara ya masuala ya kijamii katika jimbo la Lower Saxony ametoa mwito wa kupiga marufuku misalaba kwenye shule za umma. Kauli hiyo imesababisha zogo kubwa katika jimbo lake na pia ndani ya chama chake cha Christian Democratic Union kinachoiongoza serikali ya mseto ya Ujerumani.

Juu ya mwito wa waziri mteule huyo mhariri wa gazeti la Nordwest anatilia maanani kwamba kuteuliwa kwa mwanasiasa huyo mwislamu mwenye asili ya kituruki kumethibiti kuwa muhali.

Kabla ya kutoa mwito huo wa kupiga marufuku misalaba madarasani mwanasiasa huyo alitarajiwa kuwa kichocheo cha kuleta sura nzuri katika jamii kutokana na nasaba yake ya kituruki.

Gazeti la Bild Zeitung linasema,hata kabla hajaapishwa ,tayari waziri mteule huyo Aygül Özkan ameshaingia katika mvutano na waziri mkuu wake aliesema kuwa misalaba itaendelea kuning'inia madarasani.

Mhariri wa gazeti hilo pia anamkumbusha waziri mtuele Özkan kwamba uvumilivu ni sehemu ya urithi wa utamaduni wa kikristo katika jamii ya kimagharibi.

Mhariri wa gazeti la Bild anaeleza kuwa wahamiaji wanaofuata dini nyingine nchini Ujerumani pia wananufaika na uvumilivu huo.Ndiyo sababu kwamba watoto wa shule wa kituruki pia wanaruhusiwa kujitanda hijab ambazo pia waziri mteule huyo anataka kuzipiga marufuku mashuleni.

Mhariri wa gazeti la Passauer Neue Presse leo anazungumzia juu ya waumini wa dini ya kikristo waliovunjika moyo na kuamua kujitoa kanisani. Lakini mhariri huyo anasema kujitoa siyo suluhisho.Mhariri huyo anaeleza kwamba watu wanaotaka kujitoa kanisani wanapaswa kutambua kuwa ili kuweza kuleta marekebisho ndani ya kanisa ni vizuri kubakia katika kanisa. Mhariri huyo pia anatilia maanani kwamba waumini siyo milki ya maaskofu na makasisi, bali watu hao na viongozi,ndiyo kwa pamoja wanaolijenga kanisa. Kwa hiyo anaejitoa kanisani ni sawa na mtu anaejihama mwenyewe.Gazeti la Passauer Neue Presse linasema kujitoa kanisani hakutatatua tatizo lolote.

Gazeti la Dresdener Neueste Nachrichten linauzingatia mgogoro mkubwa wa madeni unaoikabili Ugiriki. Katika maoni yake mhariri wa gazeti hilo anashauri kwamba njia iliyobakia sasa ni kuisamehe madeni nchi hiyo.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen.

Imepitiwa na/ Hamidou Oummilkheir