1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri.

Abdu Said Mtullya18 Novemba 2010

Katika maoni yao wahariri wa magazeti leo wanazungumzia juu ya hatari ya ugaidi nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/QCRC
Polisi wa Ujerumani akiwa tayari kupambana na magaidi.Picha: AP

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere ametahadharisha juu ya hatari ya mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani.

Hilo ndilo suala linalozingatiwa leo na wahariri wa magazeti ya Ujerumani katika maoni yao.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linasema mpaka sasa Ujerumani imeweza kuepusha maafa ya mashambulio ya kigaidi kutokana na kazi nzuri ya idara za usalama kwa kushirikiana na idara za upelelezi za nje.Lakini aghalabu habari zinazotoka kwenye mashirika hayo ya nje siyo kamilifu na kwa hiyo ni vigumu kuzifuatilia. Ndiyo kusema kinachohitajika sasa ni kutoa tahadhari za jumla dhidi ya magaidi.

Hata hivyo mhariri wa Nürnberger anasema haitakuwa sawa kutumbukia katika kiherehere. Lakini mhariri huyo anakiri kwamba jambo hilo halitakuwa rahisi kwa baadhi ya wananchi.

Mhariri huyo anahofia kwamba baadhi ya watu wataogopa hata kupanda ndege au treni. Na wengine wanaweza hata kuepuka kuenda kwenye tafrija za Krismasi. Licha ya hayo ,mhariri anasema ni muhimu kuwa macho.

Gazeti la Saarbrücker linaunga mkono hoja hiyo japo linasema kuwa habari hizo siyo za kutia moyo. Lakini pia linasema haitakuwa sawa kwa wajerumani kuacha kuendelea na maisha yao ya kila siku kwa sababu ya kuhofia ugaidi.

Lakini mhariri wa gazeti la Westdeutsche anasema magaidi wa El Kaida wanao uwezo na nyenzo za kufanya mashambulio popote pale duniani. Na kwa hakika magaidi hao watafanya mashambulio, kwa sababu ni kwa njia hiyo tu,kwamba wataweza kukubalika kwa wafuasi wao.Mhariri huyo anasema watu hao hawana shabaha za kisiasa wala imani yoyote. Wanachotaka kuona ni damu na maangamizi tu.

Gazeti la Berliner Zeitung linauzungumzia mgogoro wa Ireland kwa kusema kuwa matatizo ya nchi hiyo yanapaswa kutoa ishara kubwa zaidi.Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kwamba umoja wa sarafu hauwezi kufanya kazi bila ya kuwepo sera za pamoja za kiuchumi na za kisiasa .Na mhariri wa gazeti la Handelsblatt anaionya Ireland kuwa kwa kadri inavyochelewa ndivyo mambo yatakavyokuwa mazito zaidi. Madeni ya nchi hiyo ni makubwa kiasi kwamba inahitaji msaada kutoka nje.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Yusuf Saumu Ramadhan/