1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya Wahariri

Sekione Kitojo9 Desemba 2010

Wahariri wanazungumzia mwisho wa mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati na kukamatwa kwa Julian Assange wa Wikileaks

https://p.dw.com/p/QU0Z
Rais Barack Obama akizungumza na waandishi habari.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani kwa kiasi kikubwa leo wameangalia masuala ya hali katika mashariki ya kati, na kukamatwa kwa mwasisi wa tovuti ya Wikileaks Julian Assange.

Tuanze na gazeti la Süddeutsche Zeitung. Gazeti linazungumzia kusalim amri kwa rais Barack Obama kuhusu amani ya mashariki ya kati. Gazeti linaandika.

Ni nini ambacho rais Obama alikihakikisha na kutoa matumaini , kwa nini hajatimiza ahadi zake za kupatikana amani katika mashariki ya kati na dunia kwa jumla, pamoja na usalama kwa ajili ya Israel. Wakati alipotunukiwa tuzo ya amani ya Nobel, kwa majigambo alitangaza kuanza tena mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati, ambapo aliahidi kuwa baada ya mwaka kutapatikana makubaliano baina ya Palestina na Israel. Baada ya hapo hakuna kitu kilichosogea. Na hivi sasa kunapatikana taarifa mpya zisizo na matumaini kutoka Marekani. Zinasema serikali ya Marekani imesalim amri, kwa kushindwa kuishawishi Israel kusitisha ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika ardhi ya Wapalestina. Kwa usahihi zaidi hii ina maana , hatua za kuleta amani zimefikia kikomo, kiongozi mwenye nguvu kabisa dunia amesalim amri kwa kundi la Walowezi wa Kiyahudi kutoka katika vilima vya Judea na Samaria.

Nalo gazeti la Der neue Tag, likizungumzia suala hilo linaandika.

Kwa ajili ya amani , hali hii iliyojitokeza sasa haifai kuharibu hatua zilizopigwa. Kwasababu huenda Wapalestina wakapata njia mpya. Wanatafuta kutambuliwa kama taifa huru. Mbinu ya mkakati huu inaelekea kuwa kama ile iliyochukuliwa na Kosovo, na Israel ilikuwa inahisi hatua hii inaweza ikachukuliwa. Hata Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel ikiwa na kura ya turufu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa haiwezi kuzuwia hatua hii, iwapo Palestina itapata uungwaji mkono wa kutosha na mataifa wanachama wa umoja wa mataifa.

Gazeti la Stuttgarter Zeitung, likitubadilishia mada linazungumzia kukamatwa kwa mwasisi wa mtandao wa Wikileaks Julian Assange. Linaadika.

Julian Assange Wikileaks Gründer
Mwasisi wa tovuti ya Wikileaks Julian AssangePicha: Picture alliance/dpa

Bila shaka mtandao wa Internet umevunja hali ya serikali, maafisa wa ngazi ya juu ama wenye viwanda na makampuni kuhodhi taarifa, na kutuweka katika mtazamo wa kidemokrasia zaidi. Lakini kupanuka kwa upatikanaji wa taarifa si suala muhimu hapa, kwa kuwa si lazima kuwa kila kinachochapishwa kinaruhusiwa. Kuchapishwa kwa nyaraka za siri katika mtandao wa Wikileaks kunatoa mtazamo wa uwezo wa kutoa mawazo na ni utambuzi wa haki ya msingi ya uhuru wa vyombo vya habari. Iwapo haki hii ipo, inaongeza hali ya utambuzi , bila kusita wa mzozo dhidi ya sheria nyingine, za ulinzi wa maeneo ya kibinafsi ama uaminifu.

Hayo ndio maoni ya wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani hii.

Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman