Maoni ya wahariri,Assad kung'atuka?
23 Agosti 2012Makamu wa Waziri Mkuu wa Syria, Kadri Djamil, alisema mjini Moscow kwamba suala la Rais Assad kung'atuka linaweza kujadiliwa. Katika maoni yake juu ya suala hilo, Mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel" anatilia maanani kwamba , huenda huo ukawa mwanzo wa kutokea mabadiliko ya kweli nchini Syria. Mhariri huyo anasema "Ishara inaonekena dhahiri. Upo wakati na mahala pa kutokea hayo. Kwani Makamu wa Waziri Mkuu wa Syria, Djalili, ameshaenda Moscow mara mbili mnamo kipindi kifupi cha wiki mbili. Ndiyo kusema kauli yake inapaswa kuzingatiwa kwa makini. Kilichobakia sasa ni kwa Rais Putin kumwalika Rais Bashar al- Assad na kumwambia abakie Urusi."
Gazeti la "Stuttgarter Zeitung" linazungumzia juu ya kupanda kwa bei ya nafaka duniani. Lakini linahoji kwamba mchakato huo hautokani tu na utengenezaji wa nishati kwa kutumia mimea na linaeleza kwamba "bei ya nafaka inapanda pia kwa sababu kiasi kikubwa kinatumika ili kuziba upungufu wa nyama. Na walanguzi nao wanachangia kwa kusababisha ugeugeu wa bei. Lakini yapasa kusema kwamba ni lazima nishati ya bio itengenezwe kwa manufaa ya kuyalinda mazingira. Ni wazi kwamba mkabala baina ya chakula na nishati utashtadi, ikiwa hayatafanyika marekebisho, na ikiwa mipaka itavukwa katika uzalishaji wa nishati kwa kutumia mazao ya kilimo." Na mhariri wa gazeti la "Kolner Stadt-Anzeiger" anaongezea kwa kusema kwamba bado upo wigo wa kuwezesha kuamua juu ya suala la nishati ya bio. Mhariri huyo anaeleza kuwa "viongozi wanaweza kuamua kati ya kutumia mimea ili kuzalisha nishati au kuchanganya na uzalisahi wa nishati kutokana na malighafi..." Na ikiwa itakuwa hivyo, hayatatokea maafa. Lakini mambo hayawezi kuwa hivyo kutokana na mgogoro wa nishati duniani. Na kwa hivyo itawezekana kukidhi mahitaji ya chakula duniani asaa ugavi, utakuwa wa haki.
Homa ya uchaguzi wa Rais inazidi kupanda nchini Marekani, kama jinsi inavyoshuhudiwa katika kauli za wanasiasa fulani. Gazeti la "Emder" linaizingatia kauli ya mwanasiasa wa chama cha Republican, Todd Akin, juu ya suala la ubakaji. Linasema: "Mwanasiasa huyo ameyasema kwa sauti kubwa yale yanayofikiriwa na watu wengi wa chama chake cha Republican." Lakini mhariri wa "Badische Neueste Nachrichten" anasema kauli ya mwanasiasa huyo wa chama cha Republican ni sawa na kujifunga goli. Todd amesema miili ya wanawake ina uwezo asilia wa kujihami dhidi ya ujazito wakati wa alichokiita ubakaji halali".
Mwandishi:Mtullya abdu/Deustche Zeitungen:
Mhariri: Miraji Othman