1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen vitani

26 Machi 2015

Wahariri wa magazeti karibu yote leo wanatoa maoni juu ya mgogoro wa nchini Yemen. Lakini pia wanatahadharisha juu ya hatari ya "Dola la Kiislamu"

https://p.dw.com/p/1Exli
Askari wa Saudi Arabia wapambana na waasi wa Kihuthi kwenye mpaka
Askari wa Saudi Arabia wapambana na waasi wa Kihuthi kwenye mpakaPicha: imago/Xinhua

Mhariri wa gazeti la Frankenpost" anatahadharisha katika maoni yake kwamba magaidi wa "Dola la Kiislamu" na wa Al - Qaeda wamekuwa wanaitumua hali ya vurumai nchini Yemen kwa manufaa yao. Na kutokana na hali hiyo litakuwa jambo la manufaa kwa Marekani na Ulaya kushikana na mshirika wao Saudi Arabia mwenye maslahi makubwa nchini Yemen.

Mhariri wa gazeti la "Frankenpost" anatilia maanani kwamba tayari makundi fulani yanaungwa mkono kifedha kupitia njia za siri. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anasema kwa manufaa ya Saudi Arabia na washirika wake,inapasa kuepusha kutokea Syria na Libya zingine karibu na Saudi Arabia.

Vita vya kiwakala

Mhariri wa gazeti la "Die Presse" anasema kinachotukia nchini Yemen ni vita vya kiwakala. Mhariri huyo anaeleza kwamba Yemen imeshatumbukia kabisa katika vurumai na sasa pana hatari kubwa ya kuzuka vita vingine vya kikanda katika eneo ambamo tayari pana mauaji nchini Syria, mapigano nchini Iraq na vita vya kupigania mamlaka nchini Libya.

Mhariri huyo anasema Yemen inakabiliwa na matatizo makubwa.Lakini kama jinsi ilivyo katika nchi zingine, matatizo hayo yanatokea ndani. Hata hivyo mhariri huyo anatilia maanani kwamba Saudi Arabia na Iran zinaendesha vita vya kiwakala nchini Yemen.

Matatizo ya ndani yanatoa mwanya kwa watu wa nje

Naye mhariri wa gazeti la "Eisencher Presse" anasema matatizo ya Yemen yapo mbali na Ulaya. Lakini mhariri huyo anaeleza kwamba siyo habari njema kusikia kwamba makundi mbalimbali yana silaha na yanavutana kupigania mamlaka katika nchi iliyogawanyika.

Mhariri wa gazeti la "Eisenacher Presse" anesema pia siyo habari nzuri kwa Saudi Arabia kuyapeleka majeshi yake nchini Yemen. Gazeti hilo linaeleza kwamba nchi zilizovurugika kaskazini mwa Afrika na kwenye eneo la ghuba, siku nyingi zimekuwa zinatumiwa kama kete katika mchezo wa sataranji. Lakini litakuwa jambo la kushtusha zaidi ikiwa magaidi wa "Dola la Kiislamu" wataingia na kujichimbia nchini Yemen.

Hatari ya "Dola la Kiislamu"

Katika maoni yake gazeti la "Die Zeit" pia lnatahadharisha juu ya hatari ya dola la kiislamu katika nchi zilizomo katika vurumai na zile zinazosambaratika. Mhariri wa gazeti hilo anasema vita vya kidini vya karne za 15 na 16 vinaendelezwa leo kwa silaha za kisasa.

Mhariri huyo anaeleza kwamba Marekani na washirika wake ,kwa kutumia tekinolojia ya kisasa, wanaweza kujaribu kuwapiga mabomu wapiganaji wa "dola la kiislamu "lakini hawataweza kuirejesha hali ya utulivu, katika eneo ambamo kila upande ni adui wa mwingine. Matumizi ya nguvu hayatasaidia mahala ambapo kwa muda mrefu palihitijika mipango mahsusi ili kuujenga uchumi na kuimarisha dola.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo