1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Kura ya Maoni ya Crimea Chanzo cha kutengwa Urusi

17 Machi 2014

Kremlin inakorofisha mambo kwa kuitisha kura ya maoni Crimea. Matokeo ya kura hiyo ya maoni sio hoja ya kuiunganisha Crimea na Urusi. Urusi imekwenda kinyume na sheria za kimataifa na imepuuza katiba ya Ukraine

https://p.dw.com/p/1BQq2
Mkuu wa Idhaa ya Kirusi ya Deutsche Welle, Ingo Mannteufel.
Mkuu wa Idhaa ya Kirusi ya Deutsche Welle, Ingo Mannteufel.Picha: DW

Rais Putin anaiongoza Urusi moja kwa moja katika katika hali ya upweke na ambayo itakuwa shida baadae kujikwamua. Kwa sababu hata China haiiungi mkono Kremlin katika sera zake za ushari kuelekea Ukraine.Utawala wa Syria tu na ule uliotengwa kimataifa wa Korea ya kaskazini ndio wanaounga mkono msimamo wa Kremlin kuelekea Crimea.

La muhimu zaidi ni ile hali kwamba wananchi hawakutoa kwa dhati maoni yao kuelekea suala la Crimea.Kura ya maoni haikuwa halali.Haikuwa huru wala ya uwazi. Kwa sababu kura hiyo ya maoni imeitishwa kwa ghafla , bila ya kuwepo mjadala wowote wa kisiasa,ina imefanyika katika hali ya kitisho iliyotokana na kuwepo wanajeshi wa Urusi walioshamiri silaha na washirika wao wa "vuguvugu la kujihami".

Hakuna anaekubali kuhadaika

Utaratibu mzima wa kura hiyo ya maoni si jambo geni,Stalin alifanya hivyo hivyo wakati na baada ya vita vikuu vya pili vya dunia katika maeneo waliyokuwa wakiyakalia ya Ulaya ya mashariki na kati. Makundi yanayoelemea upande wa Kremlin yakishirikiana na uongozi wa kijeshi mjini Moscow wameitisha kura ya maoni ya hadaa, lengo likiwa kuhalalisha mkakati wa kutaka kujipanua. Hakuna lakini aliyekubali kuhadaika.

Pengine Putin alitaraji nchi za magharibi zingezifumbia macho sera zake za kutafuta ugonvi ,zinazokwenda kinyume na sheria za kimataifa anazopanga kuziendeleza Ukraine ya baada ya enzi ya Yanukovitch. Pengine alitaraji nchi za magharibi zisingemkosoa sana. Pengine yungali bado anaamini hasira zitapungua au nchi za magharibi zitajizuwia kutangaza vikwazo. Kwa sababu kwa miaka sasa warusi wamekuwa wakiamini nchi za magharibi zinategemea kupatiwa nishati ya Urusi.

Putin ameula na chua.Na zaidi kuliko hayo uongozi wa Kremlin bado haujatambua kwamba wamekwenda mbali mno na kusababisha malumbano pamoja na nchi za magharibi na aliyeondoka patupu hapa ni Urusi yenyewe.Uchumi wa Urusi unadorora kwa sasa.Kupunguzwa thamani sarafu ya nchi hiyo Rubbels kumesababisha kupungua matumizi na kwa namna hiyo kupungua pia neema.

Vikwazo vya kiuchumi vifuatwe na vya kisiasa

Vikwazo vya kiuchumi vya nchi za magharibi vitaleta athari.Na vikwazo vya kisiasa vinaweza kutumiwa kama njia ya mwisho kuilazimisha Moscow ikubali kuzungumza na viongozi wa mjini Kiev. Huenda lakini Kremlin ikapinga na kuamua badala yake kuiunganisha Crimea na shirikisho la Urusi. Hapo hatima ya Crimea itakuwa imeshakamilika kwa upande wa Urusi lakini kwa upande wa nchi za magharibi vikwazo zaidi vinaweza kuwekwa. Na hapo Urusi haitakwepa tena kujikuta katika hali ya upweke duniani.

Mwandishi: Mannteufel,Ingo/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Khelef