1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni:Mageuzi ya kifikra yahitajika Mashariki ya Kati

Josephat Nyiro Charo13 Agosti 2014

Mageuzi yanayohitajika kuleta Mashariki ya Kati mpya yenye demokrasia lazima yatoke ndani ya eneo hilo anasema Mkuu wa Idhaa ya Kiarabu ya DW Naser Schruf.

https://p.dw.com/p/1CtKX
Gaza Waffenruhe 11.08.2014
Picha: Reuters

Katika maoni yake Mkuu wa Idhaa ya Kiarabu ya DW Naser Schruf anasema hiyo ndiyo njia pekee ya kupambana kikamilifu na makundi ya kigaidi kama vile kundi la Dola la Kiislamu la Iraq. Haujapita muda mrefu wakati ulimwengu uliposhuhudia wimbi la mapinduzi katika mataifa ya kiarabu, wakati watu waliokandamizwa walipozishinikiza tawala za kiimla zilizowatesa. Mapinduzi ya Jasmine, Mapinduzi ya msimu wa machipuko, Mapinduzi ya mtandao wa kijamii wa Facebook – haya yote ni masuala yaliyogonga vichwa vya habari katika vyombo vya mataifa ya magharibi na kwa kasi kuonekana kuashiria enzi mpya ya demokrasia na utawala wa vyama vingi Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Picha za vijana wastaarabu wa kiarabu walioandamana kwa amani zilionekana kote ulimwenguni, silaha yao pekee ikiwa ni mtandao wa mawasiliano wa intaneti, blogu na mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter. Ni nani angeweza kusahau tukio ambalo waislamu waliokuwa wakiandamana mjini Cairo nchini Misri walisali katika uwanja wa Tahrir na kulindwa kutokana na ukatili wa polisi na wenzao wakristo wa madhebu ya Coptic?

Ari na imani waliyoitumia kupigania demokrasia, uhuru, heshima ya binadamu na utangamano, furaha yao na ushujaa wao walipozigomea tawala za kiimla, yote haya yalikuwa matukio ya kweli. Na kama Mjerumani mwenye asili ya Kiarabu Naser anasema alijivunia sana.

Naser Schruf
Mkuu wa Idhaa ya Kiarabu ya DW, Naser SchrufPicha: DW

Ilieleweka kwamba wachambuzi wengi walihisi eneo jipya la Mashariki ya Kati ilikuwa likiibuka, hata kama neno "jipya" halikuwa likitumiwa wakati huo. Lakini kasi ambayo serikali za kiimla kama vile Tunisia, Misri na Yemen zilivyosambaratika, lilikuwa jambo la kushangaza sana na lilionekana kuashiria mwanzo wa enzi mpya. Lakini kipi kimebakia tangu wakati huo? Si mengi kwa kweli; Na badala yake ni kinyume kabisa cha matarajio.

Hali ni mbaya Mashariki ya Kati

Mashariki ya Kati haina taswira mpya, bali taswira mbaya. Giza totoro na hali ya sintofahamu imeugubika ulimwengu wa kiarabu. Waandamanaji wa maandamano ya msimu wa machipuko sasa wamewekwa pembeni au hata kutupwa gerezani. Badala yake vita vya wenyewe kwa wenyewe, mauaji ya safisha safisha ya kikabila, maangamizi na uharibifu ndiyo mambo yanayotawala sasa. Na katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati, sasa ni wanaume waliojihami na silaha wenye ndevu ndefu na wanaopata raha kwa kuua, ndio wenye usemi mkubwa.

Nchini Iraq na Syria, wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu, IS, sasa wanalidhibiti eneo kubwa kuliko nchi kama Jordan au Lebanon. Wamemuhangaisha na kumtisha mtu yeyote ambaye hayuko tayari kutii na kuukubali utawala wao wa sharia ya kiislamu. Haya ni mambo ya kutisha na yanayosababisha uchungu mkubwa. Ni matokeo mabovu ya mapinduzi ya msimu wa machipuko, hasa ikionekana kwamba katika maeneo mengine matatizo msingi yaliyosababisha mapinduzi hayo yametatuliwa juu juu tu. Kunahitajika mageuzi ya kifikra ili kuleta utulivu na utangamano Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Naser Schruf/Josephat Charo

Mhariri: Saumu Yusuf