1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesho kuhusu wajerumani weusi mjini Cologne

15 Novemba 2012

Jumuia ya wajerumani wenye asili ya kiafrika,Caribian na wamerekani weusi,inaandaa maonyesho yanayozunguka katika miji tofauti kuonyesha mchango wao katika jamii

https://p.dw.com/p/16jJi
Wageni wanaohudhuria maonyesho ya Homestory Deutschland mjini ColognePicha: DW/N.Schwarzbeck

Maisha ya watu ambao rangi ya mwili wao ni nyeusi yakoje nchini Ujerumani?Suala hilo lilikuwa kitovu cha maonyesho yanayozunguka kila pembe ya Ujerumani,yaliyopewa jina "Home Story Deutschland -Usimulizi wa kwetu Ujerumani-yanayoendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu wa November .Maonyesho hayo yanamulika historia ya maisha ya wajerumani wenye asili ya kiafrika au mchanganyiko wa wajerumani na wamerakani weusi.Sura ya Ujerumani hii leo inaelekea Cologne yanakofanyika safari hii maonyesho hayo.

Vicheko vimehanikiza katika ukumbi uliosheheni wa kituo cha zamani cha kikosi cha zima moto mjini Cologne.Mwimbaji wa kutoka Nigeria,Nnekka anawatumbuiza wageni kama 130 waliohudhuria sherehe za ufunguzi za maonyesho ya hayo ya Homestory Deutschland,maonyesho yanayomulika jinsi hali ya maisha ya waafrika ilivyokuwa hapo zamani nchini Ujerumani na jinsi hali hiyo namna ilivyo hivi sasa.

Manuela Ritz,bibi mmoja aliyeachia shungi la nywele ametulia juu ya kiti chake na kuangalia yanayotokea.Bibi huyo ni mmojawapo wa waandalizi wa maonyesho hayo.Manuela Ritz anatueleza jinsi wanavyowachagua wale wanaotaka kusimulia kuhusu maisha yao.

"Muhimu katika uteuzi ni kutotanguliza mbele umashuhuri.Kwa hivyo unazingatia uwanja mpana,wakiwemo watu kutoka sekta tpofauti za kazi,yaani kutoa picha ya maisha ya kawaida ya mtu mweusi."

Homestory Deutschland Ausstellung
Picha zilizotundikwa katika ubao na kutoa maelezo ya wahusikaPicha: ISD-Bund

Manuela Ritz ni mmojawapo wa waasisi wa jumuia inayojiita-vuguvugu la watu weusi nchini Ujerumani-jumuia ambayo ndiyo chanzo cha maonyesho haya kufanyika hivi sasa mjini Cologne.

Kwasababu maonyesho haya yameanza tangu mwaka 2006 na yameshazunguka katika miji kadhaa ya Ujerumani.

Miaka minne iliyopita maonyesho hayo yalifanyika pia nje ya mipaka ya Ujerumani, nchini Senegal,Uganda,Madagascar na katika nchi nyengine nane za kiafrika.Jonas Berhe amevalia suti maridadi kabisa .Anazunguka kwa madaha kutoka pembe moja hadi nyengine ya ukumbi wa maonyesho.Mjerumani huyo mwenye asili ya Eritrea ni miongoni pia mwa waandalizi wa maonyesho hayo na mwenyewe amejiwekea lengo maalum anasema:

"Tunashadidia katika maonyesho yetu, mfano unapotoa ufafanuzi katika mafunzo ya fani ya kisiasa-tunafafanua jinsi watu weusi wanavyowajibika-wakati huo huo tunapigania haki pia,tunataka kupambana na visa vya uonevu pia-tunasema,sisi sio "wengine",bali , sisi bila ya shaka huku ni kwetu kama wengine pia."

Picha 27 zimebandikwa katika ubao mweupe uliotundikwa.Katika upande mmoja wa ubao huo kuna picha ya mhusika na nyuma yake kuna maelezo kumhusu mhusika huyo.Wote hao ni kizazi cha ama mchanganyiko wa wajerumani na watu wa kutoka eneo la Caribian, mchanganyiko wa wajerumani na watu wenye asili ya Afrika au watu wenye asili ya kiafrika.Picha za zamani zaidi kati ya picha za watu hao zimepigwa katika karne ya 18 na 19-anasaema Manuela Ritz:

"Martin Dibobe amezaliwa mwaka 1876 nchini Camerun. Wimbi la ukoloni ndilo lililomleta Ujerumani na kuamua baadae kusalia na kupata kazi kama dereva wa tram.Mbele kabisa anakutikana Wilhelm Amo aliyeletwa huku kama mtumwa akiwa bado mdogo-ilikuwa kama mwaka 1706 hivi."

Picha nyengine inamuonyesha mtunga mashairi May Ayim,aliyezaliwa mwaka 1960 mjini Berlin.Katika miaka ya 80 jumuia ya watu wenye asili ya kiafrika ,Caribian au wa mchanganyiko wa wajerumani na wamarekani weusi nchini Ujerumani ilijipatia sauti kupitia vitabu vyake.Alijiuwa mwaka 1996 baada ya kushikwa na maradhi hatari.Bwana mmoja mzee hivi anaangalia kwa makini kabisa picha zilizotundukwa.Bwana huyo ni msanii Theodor Wonja Michael.Picha yake pia imetundikwa katika ubao huo mweupe pamoja na maelezo yanayozungumzia maisha yake ya kusisimua:

"Babaangu alikuja Ujerumani mwaka 1904-kama vijana wengi wa kiafrika wakati ule,kama vijana wengi wa kiafrika wafanyavyo pia hivi sasa,ambao kimsingi wanapelekwa na wazee na familia zao huku ili waje kusoma-na babaangu ilikuwa hivyo hivyo.Na bila shaka,na hilo si jambo ambalo lingeweza kuepukika,akajuana na bibi mmoja huku-akamuowa na wakazaa watoto wanne-ndugu wanne"

Theodor Wonja Michael na ndugu zake walikulia katika enzi ya tatu ya Ujerumani.Alilazimika kushiriki katika maonyesho kadhaa ya kibaguzi yanayowahusisha watu wa tamaduni za kigeni.Na alipotaka kwenda kusoma chuo kikuu,alikataliwa.Mwishoni mwa miaka ya 50 lakini akapata nafasi ya kuendelea na masomo yake.Bwana huyo mwenye umri wa miaka 87 anaishi hivi sasa mjini Cologne na ni mzee pekee wa kijerumani mwenye asili ya Afrika, au Afrodeutsche kama wenyewe watu waliozaliwa na wazee wa kijerumani na kiafrika wanavyojiita,ambae picha yake imetundikwa katika ubao mweupe wakati mwenyewe bado yu hai.

"Afrodeutsche inamaanisha mtu ana asili mbili.Yaani asili ya kiafrika na asili ya pili ni ile ya Ujerumani.Kwa hivyo mtu anapokuwa Afrodeutsche anafaidika kwasababu anajivunia tamaduni mbili.Mie nahisi hilo ni jambo la maana."

Porträt Theodor Wonja Michael
Theodor Wonja MichaelPicha: ISD-Bund

Mbali na picha hizo,maonyesho hayo ya Homestory Deutschland-au usimulizi wa kwetu Ujerumani,yanayoendelea hadi mwisho wa mwezi huu wa November yana vivutio vyengine vya kila aina .Kuanzia mihadhara,kupitia maonyesho ya tamthilia na kufikia filamu.Zaidi ya hayo watu mashuhuri wakiwemo mwaandishi habari Kena Amoa na mtangazaji wa televisheni Mola Adebis wanashiriki katika majadiliano kuhusu mchango wa watu weusi katika vyombo vya habari nchini Ujerumani.Mwezi ujao wa december maonyesho hayo yataelekea kwanza Nürnberg,katika jimbo la kusini la Bavaria na baadae Hambourg,kaskazini mwa Ujerumani.

Mbali na jumuia hiyo inayojiita vuguvugu la watu weusi nmchini Ujerumani-ISD kuna jumuia nyengine pia mashuhuri inayowaleta pamoja wanawake wa kijerumani wenye asili ya Afrika na wanawake wa kiafrika nchini Ujerumani-ADEFRA.Jumuia zote hizo makao zina makao makuu yao mjini Berlin.Kwa mujibu wa jumuia ya ISD watu hadi laki nane wajerumani wenye asili ya kiafrika wanaishi nchini Ujerumani hivi sasa.WEngi kati yao wanakutikana mjini Berlin na Hambourg.

Mwandishi:Schwarzbeck,Nadina/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu