1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utamaduni

Maonyesho mashuhuri ya vitabu mjini Frankfurt

Oumilkheir Hamidou
11 Oktoba 2017

Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamefungua maonyesho ya kimataifa ya vitabu mjini Frankfurt. Waandisahi vitabu 200 wa Ufaransa wanatembeza vitabu vyao katika maonyesho hayo ya 69 ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/2lcwQ
Deutschland Frankfurter Buchmesse 2017 Eröffnung Merkel und Macron
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamefungua maonesho mashuhuri ya kimataifa ya vitabu mjini Frankfurt. Waandisahi vitabu karibu 200 kutoka Ufaransa wanatembeza vitabu hivyo katika maonyesho hayo ya 69 ya kimataifa.

Ufaransa ndio mgeni wa heshima katika maonyesho ya mwaka huu ya vitabu yanayoendelea hadi jumapili inayokuja mjini Frankfurt. Banda la nchi hiyo jirani limeenea mita za mraba 2500 na kutembeza vitabu zaidi 40,000. Waandalizi wa maonyesho hayo makubwa kabisa ya kimataifa wanaashiria watu zaidi ya 280,000 watayatembelea maonyesho hayo yanayoyaleta pamoja mashirika zaidi ya 7,300 ya uchaposhaji kutoka zaidi ya nchi mia moja.

Bibi mmoja akifngua kurasa za kitabu katika maonyesho ya vitabu ya mjini Frankfurt
Bibi mmoja akifngua kurasa za kitabu katika maonyesho ya vitabu ya mjini FrankfurtPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Waandishi vitabu wanaashiria yanayoweza kutokea

Katika hotuba yake ya ufunguzi, kansela Angela Merkel amekumbusha mengi yanayoziunganisha Ujerumani na Ufaransa na mengi kila upande unachoweza kujifunza kutoka kwa mwenzake. "Fasihi na waandishi vitabu wanatoa mchango mkubwa kisiasa na kijamii" amesema Kansela Merkel na kuendelea:"Tunahisi kana kwamba mageuzi yanatokea kufumba na kufumbua. Na ndio maana tunashukuru tunapowaona waandishi vitabu kila mmoja akiwa na mtazamo wake, wakituonyesha jinsi wao wanavyoelewa yanayoendelea. Tunawahitaji kwa kuwa wao ndio wenye kuashiria yanayotokea.Tunawahitaji kama wabunifu na pia kama daraja katika ulimwengu tunaoshuhudia kwa sehemu jinsi nchi zinavyotegemeana lakini pia tunaona jinsi watu wanavyozidi kujifungia katika nchi na ulimwengu wao."

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ,akihutubia maonyesho ya vitabu mjini Frankfurt
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ,akihutubia maonyesho ya vitabu mjini FrankfurtPicha: picture-alliance/dpa/F. Rumpenhorst

 Utamaduni, nguzo muhimu  ya mageuzi barani Ulaya

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitiza juu ya mchango mkubwa unaoweza kutokana na utamaduni katika kuufanyia mageuzi Umoja wa Ulaya."Hakuna Ulaya bila ya utamaduni" amesema.

"Utamaduni ni njia ya maana katika kuimarisha umoja barani Ulaya, ni njia bora zaidi kuliko kuanza na shughuli za kiuchumi" amesema kwa upande wake mkurugenzi wa maonyesho ya vitabu ya kimataifa mjini Frankfurt, Jürgen Boos.

Akitilia mkazo ufanisi wa mpango wa umoja wa ulaya unaowapatia fursa wanafunzi kuendelea na masomo kwa muda wa miezi sita au zaidi katika nchi fulani ya Umoja wa ulaya-Erasmus, rais Macron ameelezea matumaini yake kuwaona nusu ya vijana wa Ufaransa wenye umri wa chini ya miaka 25 wakenda kuendelea na masomo katika nchi nyengine ya Umoja wa Ulaya. Ni muhimu kwa vijana kujifunza lugha zaidi ya mbili amesema.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AF

Mhariri: Mohammed Khelef