1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri waahidi kuimarisha mapambano

Admin.WagnerD21 Julai 2016

Mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya nje kutoka nchi zaidi ya 30, wanaokutana mjini Washington wameelezea wasi wasi juu ya ombwe linaloweza kutokea baada ya sehemu zinazokaliwa na Dola Kiislamu magaidi kukombolewa

https://p.dw.com/p/1JTpY
Mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wa Marekani John Kerry
Mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na wa Marekani John KerryPicha: Reuters/J. Roberts

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter amesema kilichozungumziwa zaidi mpaka sasa ni juu ya ujenzi mpya wa sehemu hizo.Waziri Carter amesema nchi zilizofungamana dhidi ya Waislamu wenye itikadi kali wa "Dola la Kiislamu" zinadhamiria kuimarisha mapambano dhidi ya magaidi hao.

Amesema wataendelea kutafuta njia za kuongeza kasi kama ambavyo wamekuwa wanafanya wakati wote ili kuwachakaza kabisa wapiganaji wa "Dola la Kiislamu".

Mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya nje kutoka nchi zaidi ya 30 wanakutana mjini Washington kujadili hatua zaidi zinazoweza kuchukuliwa ili kuwashinda magaidi wa Dola la Kiislamu. Lakini pia wameelezea wasiwasi juu ya pengo linaloweza kutokea baada ya miji na sehemu zinazokaliwa na magaidi hao kukombolewa nchini Syria na Irak.

Baada ya kikao cha siku ya kwanza Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter amesema mazungumzo yalituwama zaidi juu ya juhudi za ujenzi mpya wa miji na sehemu hizo. Carter amesema wasi wasi mkubwa wa nchi hizo 30 ni juu ya hatua za kuleta utulivu na utawala imara katika sehemu zitakazokombolewa.Amesema ana wasi wasi huenda hatua hizo zikalegalega nyuma ya harakati za kijeshi.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter
Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton CarterPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeier amesema mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh bado hayajamalizika kwa hivyo nchi hizo zinapaswa kuutimiza wajibu wa kibinadamu na wa kisiasa katika kuwakomboa watu nchini Irak na Syria waondokane na utumwa unaowasibu chini ya "Dola la Kiislamu".

Waziri wa ulinzi wa Uingereza Michael Fallon amezitaka nchi zilizofungamana dhidi ya "Dola la Kiislamu" zihakikishe kwamba zinaendelea kuiunga mkono serikali ya Iraq katika mapambano yake dhidi ya magaidi wa Daesh, baada ya mji wa Mosul kukombolewa kabisa.

Hata hivyo juu ya Syria kiongozi wa pande za upinzani zilizofungamana dhidi ya utawala wa Bashar al- Assad ametoa mwito wa kuyasimamisha mashambulio ya anga yanayoongozwa na Marekani dhidi ya "Dola la Kiislamu" wakati ripoti juu ya vifo vya raia kadhaa katika mji wa kaskazini wa Manbij inachunguzwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya asasi inayofuatlia haki za binadamu nchini Syria, watu wasiopungua 56 waliuawa katika mji huo hapo juzi kutokana na mashambulio ya ndege. Wakati huo huo, kwenye mkutano wao, mjini Washington, wafadhili kutoka nchi kadhaa wameahidi kutoa kiasi cha dola Bilioni 2 kwa ajili ya kuisaidia Iraq na wakimbizi wa Syria.

Mwandishi:Mtullya abdu/ ape,rts

Mhariri: Caro Robi