1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano dhidi ya Malaria bila ya DDT

12 Mei 2009

WHO kupunguza matumizi ya DDT.

https://p.dw.com/p/HokL
Mbu anayeambukiza ugonjwa wa MalariaPicha: DW-TV


Wakati umuhimu unatiliwa katika huduma za afya kwa jamii, hasa wakati huu tunapoushuhudia ugonjwa wa homa ya nguruwe, hata hivyo, juhudi zinafanywa kimya kimya kutokomeza kitisho kinachjoendelea kuweko cha ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa wa Malaria unawaua karibu watu milioni moja kila mwaka. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO; na karibu nusu ya wakaazi wa dunia wako katika hatari ya kuupata ugonjwa huo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Mazingira, UNEP, Shirika la Dunia la kutoa nafasi kwa mazingira, Global Environment Facility, na Shirika la WHO wiki iliopita yalitangaza miradi kumi ambayo itapambana na ugonjwa wa Malaria, huku kidogokidogo kukiachwa mtindo wa kutegemea dawa ya DDT katika kuwauwa mbu wanaobeba vimelea vya Malaria. Matumizi ya dawa hiyo ya DDT yamesababisha mabishano. Mwaka 2006, Shirika la WHO lilitoa ilani ya tahadhari katika jamii ya walinzi wa mazingira kwa kuunga mkono sana kunyunyizwa dawa hiyo katika maeneo ndani ya majengo. Hiyo ilionekana kuachana na msimamo wa hapo kabla wa kukubali zaidi kutumiwa dawa hiyo.


Lakini tangazo la wiki iliopita liliwakilisha yale yalioitwa matarajio kwamba dawa hiyo ya DDT itapunguwa kutegemewa kutumiwa katika siku za mbele. Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dr. Margret Chan, amesema shirika lake linakabiliana na mitihani miwili: nia ya kufikia lengo la kupunguza sana mzigo wa magonjwa yanayoambukizwa na vijidudu, hasa Malaria, na, wakati huo huo, kuwa na nia ya kufikia lengo la kupunguza kuitegemea DDT katika kuzuwia magonjwa hayo yanayoambukizwa na vijidudu.


Tangazo hilo lilikuja katika mkutano wa nne wa pande zinazohusika na Mkataba wa Stockholm juu ya madawa yanayoharibu mazingira ya mimea huko Geneva. Chini ya mkataba wa Stockholm, uliokubaliwa mwaka 2001, DDT na madawa mengine 11 yalipigwa marufuku, japokuwa DDT iliruhusiwa kutimiwa katika kupambana na ugonjwa wa Malaria. Lakini afisa mmoja wa Shirika la WHO amesema shirika lao bado linaambatana na makubaliano ya Stockholm. Alisema wao wanapendekeza kutumiwa DDT katika baadhi ya mikasa ya magonjwa ya Malaria pale hakuna mbadala.


Miradi hiyo iliotangazwa na WHO itafanyika katika nchi 40 barani Afrika, nchi zilioko mashariki ya Bahari ya Mediterrenean na Asia ya Kati. Miradi hiyo imepewa dola milioni 40 kutoka Global Environment Facility, na inatarajiwa kwamba DDT itapunguka kutumiwa kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2014, na dunia kuwa huru na matumizi ya DDT ifikapo mwaka 2020. Miradi hiyo itaanza mwakani na kudumu miaka mitano.


Jamii ambazo zimekuwa zikitegemea kwa miaka 50 kutumia unyunyizaji wa madawa ya DDT katika vidimbwi vya maji ili kuzuwia Malaria zilianza kutumia njia nyingine, kama vile kupanda miti inayofukuza mbu, kukausha maeneo ambapo maji yanatwama, kutumia samaki wanaokula mayai ya mbu na kuziba madirisha na milango kwa nyavu. Maghala ya kuwekea DDT na madawa mengine ya mimea yalijengwa na mirundiko ya madawa hayo itaangamizwa. Mbinu hizo zisizokuwa za kikemikali, pamoja na mikakati mingine inayosimamiwa na watu wenyewe, imesaidia kupunguza visa vya kuambukizwa na ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 60.


Afrrika Kusini ilikuwa moja wapo ya nchi za mwanzo kutumia DDT katika kupambana na Malaria, na iliweza kwa haraka kupunguza maeneo yalioathirika na ugonjwa huo. Pale madawa mbadala yalipotumiwa, hata hivyo, mbu wenye kubeba Malaria waligeuka kuwa masugu wa dawa.


Hata hivyo, inatarajiwa kwamba maendeleo sambamba yanaweza yakapatikana katika kupunguza matumizi ya DDT na pia idadi ya watu wanaouguwa Malaria, hivyo kupelekea njia endelevu ya kupambana na ugonjwa huo.


Mwandishi: Othman Miraji

Mhariri: Mohamed Abdulrahman