1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano ya Aleppo yaendelea

31 Julai 2012

Mapambano makali katika mji wa Aleppo, Syria, yanaingia siku yake ya 11 licha ya kuwepo kwa lawama za kimataifa dhidi ya serikali ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa ukisema zaidi ya watu 200,000 wameshaukimbia mji huo.

https://p.dw.com/p/15gzj
Waasi wa Jeshi la Syria Huru wakijipanga kupambana na jeshi la serikali mjini Aleppo.
Waasi wa Jeshi la Syria Huru wakijipanga kupambana na jeshi la serikali mjini Aleppo.Picha: Reuters

Wanaharakati wanaripoti kupigwa kwa mabomu katika viunga vinavyoshikiliwa na waasi na mapigano ya risasi katika sehemu nyingi za Aleppo.

Haya ni makabiliano yaliyochukuwa muda mrefu zaidi kuliko yale ya mji mkuu Damascus, mapema mwezi huu, huku waasi wakidai kupata ushindi katika maeneo kadhaa ya mji huo mkubwa kabisa nchini Syria na wenye wakaazi wapatao milioni tatu.

Alfajiri ya leo, waasi walifanya mashambulizi dhidi ya ofisi ya chama tawala cha Baath katika wilaya ya Salhin na mahakama ya kijeshi na makao makuu ya jeshi la anga katika wilaya ya Zahraa.

Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, viunga vya Salahuddin, Marjeh, Firdoss, Al-Mashhad, Sakhur, Al-Shaar na Ansari vilishambuliwa kwa mizinga ya majeshi ya serikali usiku mzima, huku waasi wakikabiliana na wanajeshi hao katika viunga vya Al-Meesr na Al-Adaa.

Eneo la karibuni kabisa kutekwa na waasi ni Al Bab, ambacho ni kituo muhimu cha uangalizi wa kijeshi katika jimbo la Anand, mpakani mwa Syria na Uturuki.

Jeshi la Syria latumia vifaru na helikopta

Jeshi la Syria linaripotiwa kutumia helikopta na vifaru katika operesheni hii kubwa ya kuudhibiti tena mji huo, huku serikali ikiitetea operesheni hiyo mbele ya Umoja wa Mataifa, ikiulezea mji wa Aleppo kuwa umo kwenye "mikono ya magaidi mamluki wanaofadhiliwa na Qatar, Saudi Arabia na Uturuki, na ambao wanawashikilia raia kama ngao na kufanya uhalifu wa kutisha."

Waasi wa Syria wakiwa kwenye gari kuelekea mstari wa mbele wa mapigano ya Aleppo.
Waasi wa Syria wakiwa kwenye gari kuelekea mstari wa mbele wa mapigano ya Aleppo.Picha: AP

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ameelezea wasiwasi wake juu ya matumizi ya silaha hizo nzito, na kuzitaka pande zote mbili kusitisha mapigano.

Hapo Jumapili timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa unaofuatilia utekelezwaji wa mpango wa amani wa mjumbe wa kimataifa, Kofi Annan, ilisema msafara wa Luteni Jenerali Babacar Gaye ulishambuliwa kwa bunduki katika mji wa kati wa Homs.

"Msafara wa Jenerali Gaye ulishambuliwa. Kama munavyojua zaidi ya magari kumi ya ya Umoja wa Mataifa yameshambuliwa na kuharibiwa kabisa. Ni bahati nzuri tu kwamba hakuna aliyejeruhiwa katika mashambulizi haya." Amesema Ban Ki-moon.

Ban Ki-moon amesema kwamba zaidi ya watu milioni mbili wameathirika na mapigano katika nchi hiyo yenye raia milioni 12, akiongeza kwamba "mapigano zaidi si suluhisho."

Katika mji wa Aleppo peke yake, Umoja wa Mataifa unakisia kwamba zaidi ya watu 200,000 wamekimbia mapigano na sasa aidha wamejificha kwenye vijiji vya karibu au katika makambi ya wakimbizi nchini Uturuki.

Wakimbizi kutoka Aleppo wameuelezea mji wao kama unaoporomoka.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman