1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano yanaendelea Libya

30 Septemba 2011

Umoja wa mataifa na duru nyengine zimeripoti kuwa raia wanaukimbia mji uliozungukwa wa Sirte nchini Libya ambako mapigano ya kuwaondoa wafuasi wa Muammar Gaddafi, yamesababisha vifo vya watu wengi

https://p.dw.com/p/12jZU
Wapiganaji wa upinzani Libya wanapambana na wafuasi wa GaddafiPicha: dapd

Umoja wa mataifa na duru nyengine zimeripoti kuwa raia wanaukimbia mji uliozungukwa wa Sirte nchini Libya ambako mapigano ya kuwaondoa wafuasi wa kiongozi aliyepinduliwa, Muammar Gaddafi, yamesababisha vifo vya watu wengi.

Kämpfe in Libyen Bani Walid
Mji wa Sirte umezungukwaPicha: dapd

Wakati huo huo, viongozi wapya nchini humo hii leo wamekuwa wakichunguza taarifa kuhusu kukamatwa kwa msemaji wa Gaddafi, Mussa Ibrahim, katika mapambano hayo yanayoendelea.

Vikosi vya serikali ya mpito Libya hapo jana viliudhibti kwa mara nyengine uwanja wa ndege mjini Sirte, sehemu ambako wafuasi wa Kanali Muammar Gaddafi wamekuwa wakitumia wadenguaji, maroketi na bunduki za rashasha, katika mashambulio makali ya kujaribu kuzuia udhibiti wa mojawapo ya maeneo mawili makuu wanayoyadhibiti.

Lakini kuendelea kwa muda mrefu mapigano hayo katika mji huo alikozaliwa Gaddafi, yamezusha wasiwasi unaozidi, kwa raia kiasi ya laki moja waliokwama ndani ya mji huo, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa kuyahatarisha maisha ya raia hao.

Kwa mujibu wa duru ya Umoja wa mataifa, serikali ya mpito nchini humo imeuomba Umoja huo wa mataifa kuwasaidia na mafuta ya kujaza kwenye magari ya kubebea wagonjwa ambayo yatatumika kuwahamisha wapiganaji waliojeruhiwa kutoka Sirte.

Aliongeza kuwa Umoja huo unatuma magari na maji ya kunywa kwa idadi kubwa inayoongezeka ya raia wanojikusanya katika magari na kuukimbia mji huo wakielekea Benghazi, mashriki au mjini Misrata, magharibi.

Sirte Libyen 15.09.2011
Picha: dapd

Lakini mapigano mjini humo na kuzidi kutokuwepo usalama katika mji wa Bani walid, mji wa pili unaodhibitiwa na wafuasi wa Gaddafi, yanazuia Umoja huo wa mataifa kutuma wafanyakazi wake wa kutoa misaada ndani ya mji huo.

Wakati huo huo, makamanda wa baraza la mpito la kitaifa Libya, NTC wamesema wamepokea taarifa kutoka kwa wapiganaji waliopo vitani kuwa msemaji wa Gaddafi, Mussa Ibrahim, alikamatwa nje ya mji wa Sirte, sehemu ambayo wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani wamezungukwa kwa muda wa wiki sasa.

Bürgerkrieg in Libyen Erfolg der Rebellen
Msemaji wa utawala wa Gaddafi Moussa IbrahimPicha: dapd

Lakini kamanda wa wapiganaji hao aliyepo mjini Misrata, Mustafa bin Dardef, amesema hakuna uwezo wa kuthibitisha kukamatwa kwa Mussa Ibrahim, ambaye amekuwa akitoa ujumbe wa kuunga mkono utawala wa Gaddafi kutoka maeneo yasiojulikana huku akiwa anaendelea kukimbia upinzani nchini humo.

Kamanda mwingine, Mohammed al Marimi, alisema Mussa alikamatwa na wapiganaji wa kutoka Misrata alipokuwa akiendesha gari nje ya mji wa Sirte, na kuwa kuna ripoti zisemazo kuwa msemaji huyo alikuwa amevalia nguo kama mwanamke. Taarifa ambazo amesema hawezi kuzithibitisha moja kwa moja.

Kituo cha televisheni nchini humo, Al Hurra Misrata, kimesema kitaonyesha kanda za video zinazoonyesha kukamatwa kwa Ibrahim na kuongeza kuwa picha hizo zilimuonyesha akiwa amezuiliwa nyuma ya gari nje ya Sirte akiwa amevalia bui bui.

Katika siku za hivi karibuni msemaji huyo hajatoa ujumbe wowote kama ilivyokuwa kawaida yake, tangu wapiganaji wa baraza la mpito kuudhibiti mji wa Tripoli.

Mwandishi:Maryam Abdalla/Afpe
Mhariri:Josephat Charo