1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAPATANO,CANCUN.

Abdu Said Mtullya11 Desemba 2010

Mapatano yafikiwa Cancun juu ya kupunguza gesi hatari.

https://p.dw.com/p/QVvQ
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwenye mkutano wa Cancun.Picha: AP

Wajumbe kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Cancun,Mexico uliojadili njia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani, leo wameupitisha mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuanzisha mfuko mpya wa fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini.

Mpango huo umepitishwa licha ya upinzani wa Bolivia.

Waziri wa mambo ya nje wa Mexico Patricia Espinosa aliwaambia wajumbe baada ya mazungumzo ya wiki mbili kwamba makubaliano hayo ni zama mpya katika ushirikiano wa kimataifa katika juhudi za kukabiliana na mabadiliiko ya hali ya hewa.

Hata hivyo mazungumzo hayo mjini Cancun yaligubikwa na mabishano baina ya nchi tajiri na masikini.

Makubaliano yaliyofikiwa leo yanajumlisha Mfuko wa fedha, unaoitwa "Mfuko wa Kijani " pia unasisitiza lengo la kupatikana dola Bilioni mia moja za msaada hadi utakapofika mwaka wa 2020.

Mpango huo pia unajumlisha hatua za kuilinda misitu katika nchi za joto na njia mpya za kupeana tekinolojia mpya za nishati.

Waziri wa mambo ya nje wa Mexico bibi Espinoza aliufunga mkutano baada ya kupiga nyundo mezani kuashiria kwamba mapatano yamefikiwa licha ya upinzani wa Bolivia.Mjumbe wa nchi hiyo amesema kwamba makubaliano yaliyofikiwa hayaziwajibishi nchi tajiri kwa kiwango cha kutosha katika kupunguza gesi zinazoharibu mazingira.