1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapato ya mauzo ya bidhaa Ujerumani kupungua

3 Septemba 2009

Wataalamu wanasema kutaathiri ukuaji uchumi

https://p.dw.com/p/JOTE
Wateja katika duka moja mjini Hamburg.Picha: dpa

Kuimarika kwa mauzo na ununuzi bidhaa wa wateja kulikotokeza katika hali ya kushangaza licha ya msukosuko wa kiuchumi duniani, huenda kukapungua mnamo miezi michache ijayo. Inasemekana hayo yatatokana na watu kurejea katika kuweka akiba zaidi kuliko kutumia fedha zao, na hivyo kuuacha uchumi utegemee nyanja nyengine zinazokuza uchumi.

Matumizi ya vitu vya nyumbani yalisaidia kuupiga jeki uchumi wa Ujerumani, ulio mkubwa kabisa barani Ulaya na kuweza kujitoa katika hali mbaya katika robo ya pili ya mwaka huu. Kuongezeka kwa mauzo mnamo mwezi uliopita wa Agosti kukaonyesha kwamba Wajerumani bado wanamiminika kwa wingi madukani pamoja na msukosuko wa kiuchúmi duniani.

Lakini hali hiyo ilikua na sababu zake ambazo miongoni mwazo ni utulivu wa bei za bidhaa na utaratibu maalum wa serikali kutoa ruzuku kwa watakaoachana na magari yao ya zamani yaliotimia miaka 9 au zaidi, ili kununua jengine au hata jipya kabisa. Utaratibu huo ulikua wa muda maalum na ulimalizika Jumatano ya wiki hii.

Aidha mpango ulioungwa mkono na serikali wa kupunguza muda wa masaa ya kazi, pia ulisaidia kupunguza idadi ya wasio na ajira na hivyo kuimarisha mauzo ya bidhaa. Hivi sasa yote hayo yanafifia na ni katika wakati ambao uchumi ndiyo kwanza umeanza kukua.

Peter Hohlfeld, mchambuzi wa masuala ya uchumi katika taasisi ya Hans Boeckler anasema, anasema kumalizika kwa ule muda uliowekwa wa ruzuku kufidia ununuzi wa gari mpya, kumesababisha kuongezeka tena kwa idadi ya wasio na ajira.

Hadi wateja milioni mbili walihusika na mpango huo na serikali ikatangaza kwamba ruzuku hiyo ya jumla ya euro bilioni 5 sasa imeamalizika.

Sambamba na hayo, uzoefu wa siku za nyuma unaonyesha vipi wanunuzi walivyoguswa na mabadiliko ya bei. Mauzo ya reja reja yalipanda kwa asili mia 6.3 katika mwezi wa Januari 2007 wakati serikali ilipoongeza kodi aya mauzo kwa asili mia tatu.

Wajerumani walianza kufurahia mazingira mazuri ya bei mwaka huu, ambayo yamesaidia kuinua kiwango cha mauzo kwa jumla. Ughali wa maisha uliweza kudhibitiwa. Matumizi ya nyumbani yameimarika pia kutokana na ongezeko la mishahara lililokubaliwa mwaka jana, lakini Reinhard Bispinck ambaye pia ni mtaalamu katika taasisi ya Hans Boeckler anasema ongezeko la mishahara katika nusu ya mwaka huu ilifikia hadi asili mia 3 kwa mwaka.

Lakini pamoja na hayo anasema mtindo wa waajiri kutumia ajira ya muda wa masaa machache, ni mtindo uliomeza sehemu kubwa , kiti cha fedha ambacho hatimae mfanyakazi anakwenda nacho nyumbani.

Ofisi ya takwimu ya Shirikisho imesema idadi ya wasio na ajiara ilipungua kwa 34.000 mwezi Julai lakini wanauchumi wanatarajia ukosefu wa ajira kuongezeka na kuwa zaidi ya milioni 4 mwaka ujao, baada ya kushuka kidogo hadi karibu milioni 3 , mia nne sabini na mbili elfu mwezi uliopita wa Agosti.

Biashara iliimarika mno mwezi uliopita kufikia kiwango kikubwa kuwahi kuonekana kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita na kuzusha matumaini kwamba Ujerumani itaongoza juhudi za kufufua uchumi miongoni mwa mataifa yanayotumia sarafu ya euro, kutokana na kuimarika usafirishaji wa bidhaa zake nje.

Serikali itakayoingia madarakani baada ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi huu nchini Ujerumani, huenda ikajaribu tena kuwaraia Wajerumani waondokane na tabia ya kuweka akiba na badala yake kutumia, ili kuimarisha uchumi. Kusaka njia za kuwashawishi wateja kufanya hivyo, bila shaka , itakua ndiyo changa moto kubwa kwa serikali mpya.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman/RTRE

Mhariri:Sekione Kitojo.