1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali yaitikisa Aleppo

4 Mei 2016

Mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Syria yamehamia mjini Berlin hii leo ambapo Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anakutana na mjumbe wa usuluhishi wa Syria Staffan De Mistura.

https://p.dw.com/p/1IhYn
Syrien Zerstörung in Aleppo
Picha: Reuters/A. Ismail

Mapigano makali yameendelea usiku wa kuamkia leo baina ya vikosi vya waaasi na wanajeshi wa serikali katika mji wa pili kwa ukubwa wa Aleppo nchini Syria huku raia wakipoteza maisha.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier atakutana na mjumbe wa usuluhishi wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria Staffan de Mistura, na kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Riad Hijab pamoja na mwanadiplomasia wa juu kutoka nchini Ufaransa Jean-Marc Ayrault mjini Berlin kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mazungumzo ya dharura hii leo juu ya mzozo huo ikiwa ni baada ya wito wa kuchukua hatua zaidi kutolewa na Ufaransa na Uingereza. Naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameuonya utawala wa Bashar al-Assad kwa kuanzisha mapigano mapya wakati mazungumzo yakusitisha mapigano hayo yakiendelea mjini Berlin.

Kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa haki za binadamu nchini humo , Muungano wa makundi ya upinzani yanayopigana chini ya jina la "Fatah Halab" yalishambulia vikosi vya serikali ya Bashar al-assad kwa kurusha bomu katika tanuri.

John Kerry akiwa na msuluhishi Staffan de Mistura
John Kerry akiwa na msuluhishi Staffan de MisturaPicha: Reuters/D.Balibouse

Vikosi hivyo vya waasi vimeendelea kusogea katika vitongoji vya mitaa inayoshikiliwa na serikali , hata hivyo vikosi vya serikali vimefanikiwa kuwasogeza nyuma asubuhi ya leo. Mapigano makali yamesikika usiku kucha yakiwemo makombora na mashambulizi ya angani.

Mkuu wa shirika hilo la uangalizi wa haki za binadamu Rami Abdel Rahman amesema mapigano ya usiku kucha yalikuwa makali kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha mwaka mmoja. Mapigano hayo ya wiki mbili mjini Allepo tayari yamepoteza maisha ya raia 270. Waasi wanasema kuwa wamewaua wapiganaji wa serikali wapatao 40 wakati huo idadi ya waasi waliopoteza maisha ikifikia watu 10. Shirika la habari la nchini humo limeripoti kuwa raia watatu wameuawa asubuhi ya leo wakati waasi waliporusha kombora katika eneo linaloshikiliwa na serikali.

Tangu mwaka 2012 , mji wa Allepo umegawanyika katika maeneo mawili , eneo la Magharibi likishikiliwa na serikali huku lile la Mashariki likishikiliwa na waasi.

Hali inavyoonekana mjini Allepo
Hali inavyoonekana mjini AllepoPicha: Reuters/A. Ismail

Mpaka sasa jumla ya raia 270000 wameuawa na mamilioni wakiyakimbia makazi yao tangu kuanza kwa mzozo nchini syria mwaka 2011.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Yusuf Saumu