1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya Sudan yanazidi kulididimiza taifa hilo

Lilian Mtono
10 Agosti 2023

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema mapigano ya Sudan yaliyodumu kwa karibu miezi minne yanazidi kulididimiza taifa hilo, huku mamilioni ya watu wakiwa wanakabiliwa na janga la kibinaadamu.

https://p.dw.com/p/4V0tZ
Sudan Trümmer nach Angriffen in Khartum
Baadhi ya nyumba zilizoharibiwa kwenye mzozo nchini SudanPicha: AP Photo/picture alliance

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema mapigano ya Sudan yaliyodumu kwa karibu miezi minne yanazidi kulididimiza taifa hilo, huku mamilioni ya watu wakiwa wanakabiliwa na janga la kibinaadamu na uwezekano wa mzozo mpya wa kikabila unaosambaa nchini humo.

Wakisoma muhtasari kuhusiana na hali hiyo mbaya, msaidizi wa katibu mkuu wa umoja huo Martha Phoebe, pamoja mkurugenzi wa operesheni Edem Wosornu, wameelezea hali mbaya iliyosababishwa na kusambaa kwa machafuko huku kukiwa hakuna dalili ya kufika mwisho.

Kulingana na serikali, zaidi ya watu 3,000 wamekufa hadi kufikia mwezi Juni kutokana na mzozo huo.

Wosornu amesema kitisho cha taifa hilo kutumbukia katika mzozo kamili wa kibiaadamu kimeongezeka, wakati zaidi ya watu milioni 4 wakiwa wameyakimbia makazi yao na zaidi ya milioni 20 wakikabiliwa na kiwango cha juu cha uhaba wa chakula wa ama njaa kali.