1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya wapalestina yanachafua mustakabali wa taifa lao.

Sekione Kitojo19 Mei 2007

Ni hali ya uchungu mkubwa anayohisi mwanasiasa veterani akiangalia watu nchini mwake wakivurugana na kuuwana, lakini hana la kufanya. Kile kinachotokea katika eneo la Gaza kinahatarisha sio tu serikali ya umoja wa kitaifa, lakini pia mshikamano wa kijamii, lengo la Palestina na mkakati wa Palestina kwa jumla, alisema kwa masikitiko makubwa Saeb Arakat, mshirika wa karibu wa rais wa Palestina Mahmoud Abbas na mjumbe wa muda mrefu katika majadiliano na Israel.

https://p.dw.com/p/CHE6
Waziri wa mambo ya kigeni wa mamlaka ya Palestina Ziad Abu Amr (k) akiwa na waziri mwenzake wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier baada ya mazungumzo yao mjini Berlin hivi karibuni.
Waziri wa mambo ya kigeni wa mamlaka ya Palestina Ziad Abu Amr (k) akiwa na waziri mwenzake wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier baada ya mazungumzo yao mjini Berlin hivi karibuni.Picha: AP

Erekat alikuwa akizungumzia kuhusu ghasia za kimakundi baina ya Hamas na Fatah kuwa kwa mara nyingine tena zimetamalaki katika ukanda wa Gaza, na kusababisha watu kadha kuuwawa katika muda wa wiki moja iliyopita na kuwaacha wakaazi wa eneo hilo wakiwa wenye hofu hata ya kutoka majumbani mwao huku mapigano katika mitaa yakiendelea.

Kuingia kwa Israel katika mapigano hayo, kwa njia ya kulenga wapiganaji wa Hamas kwa kulipiza kisasi kutokana na kurushwa kwa makombora darzeni kadha kutoka katika ukanda huo wa pwani ndani ya Palestina kunatishia kukoroga mambo zaidi.

Katika tukio baya kabisa wiki iliyopita , walinzi watano wa Fatah walipigwa risasi na kufa wakati wapiganaji wa Hamas walipovamia nyumba ya kiongozi wa ngazi ya juu wa masuala ya usalama katika chama cha rais Mahmoud Abbas mjini Gaza. Rashid Abu Shbak na familia yake hawakuwapo nyumbani wakati huo wa shambulio. Saa chache baadaye wapiganaji wa Hamas walirusha makombora katika viwanja vya vya ofisi ya Abbas mjini Gaza.

Katika mitaa wapiganaji kutoka makundi hayo hasimu, wakiwa wamevalia vitambaa vyeusi usoni na bunduki mkononi , walikuwa wamejiweka katika nafasi zao katika maeneo ya makutano ya njia.

Mapigano hayo baina ya Hamas na Fatah ni mabaya zaidi tangu walipouwawa zaidi ya Wapalestina 100 katika mapambano yaliyozuka baina ya makundi hayo mawili mjini Gaza mwaka huu. Duru hiyo ya ghasia ilimalizika baada ya makubaliano kupatikana mjini Mecca yakisimamiwa na Saudi Arabia , ambayo iliweza kuwashawishi Hamas , chama ambacho kilishinda uchaguzi wa bunge mapema mwezi Januari 2006 ,kugawana madaraka na Fatah.

Lakini muundo wa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa ulikuwa tayari na dosari toka mwanzo kutokana na suala la udhibiti wa majeshi ya usalama kuwa halikutatuliwa, na kupanda mbegu ya ghasia za hivi sasa, amesema Ely Karmon mtafiti mwandamizi katika kituo cha nadharia mbali mbali kilichoko Herzliya, kaskazini ya mji mkuu wa Israel Tel Aviv.

Karmon anadokeza kuhusu udhaifu wa uongozi wa kisiasa wa Palestina na mgawiko ndani ya Fatah na Hamas , alipokuwa akielezea kuhusu kushindwa kwa juhudi za sasa za kumaliza ghasia.

Machafuko ya Gaza hata hivyo hayawezi kuelezewa kirahisi tu kuwa ni mapambano kati ya Fatah na Hamas.

Katika mapigano ya hivi karibuni , majeshi ya Hamas ambayo yana silaha za kutosha yamekuwa yakipata ushindi, huku majeshi ya Fatah yakipata hasara kubwa. Kumekuwa na ripoti siku ya Ijumaa katika gazeti la kila siku la Haaretz nchini Israel kuwa maafisa wa usalama wa mataifa ya magharibi wameitaka Israel kumpatia mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas nyenzo anazohitaji ili kupambana na Hamas, kwanza kabisa , ikiwa ni uwezo wa kuwalipa wanajeshi wake mishahara. Lakini kuingilia kati kwa Israel kwa niaba ya Fatah kunamdhoofisha zaidi Abbas, ambaye ataoneka kuwa ni kibaraka wa Israel na mataifa ya magharibi.

Tayari wiki iliyopita , baada ya kuwa na ripoti kuwa Fatah kimeomba kupatiwa vifaa vya kijeshi, msemaji wa Hamas amelishutumu kundi hilo kwa kuwa vibaraka wa mataifa ya magharibi.

Shutuma kama hizo zimeelekezwa pia kwa Israel, kwa Hamas kurusha maroketi yake dhidi ya Israel na Israel nayo kuanza kuwashambulia wanachama wa kundi hilo mjini Gaza.

Njia pekee ya kuondokana na ghasia huko Gaza ni iwapo kundi la watendaji wa Hamas watakubali kuungana na Fatah, huenda hapo kutakuwa na nafasi ya amani.