1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea Libya kudhibiti bandari ya Misrata

27 Aprili 2011

Nchini Libya, katika mapigano ya kuudhibiti mji wa Misrata, vikosi vya serikali nchini humo vimerejea nyuma baada ya kushambuliwa na ndege za kijeshi za Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

https://p.dw.com/p/RKdd
Neighbours examine the damage to a house which was struck by a shell in Misrata, Libya, Monday, April 25, 2011. Gadhafi's troops on the outskirts of Misrata unleashed more shells into the city Monday, hitting a residential area and killing 10 people, including five members of one family, according to a doctor in Misrata. (AP Photo)
Nyumba iliyobomolewa na kombora mjini MisrataPicha: AP

Hata hivyo, wanajeshi hao wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi wameanza kulishambulia upya eneo la bandari ya Misrata. Bandari hiyo ni muhimu sana kwa pande zote mbili, kwani hiyo ni njia inayotumiwa kupitisha misaada ya kijeshi na kibinadamu kwenda kwa waasi wanaopigana na vikosi vya serikali ya Libya katika eneo la Magharibi nchini humo. Lengo la Gaddafi ni kuukomesha uasi wa wapinzani wake wanaotaka umalizike utawala wa miongo minne wa Gaddafi. Lakini licha ya mapigano ya majuma kadhaa, si vikosi vya Gaddafi wala waasi wanaosaidiwa kwa mashambulizi ya anga ya NATO, chini ya uongozi wa Uingereza na Ufaransa, walioweza kupata ushindi wa maana.

Jumuiya ya kimataifa yagawika

Mapigano yanayoendelea kati ya waasi na vikosi vya serikali ya Libya, bila ya upande wo wote kushinda, yanadhihirisha jinsi jumuiya ya kimataifa inavyoendelea kugawika pande mbili. Upande mmoja, wakosoaji wa mashambulizi ya NATO, wanasema kuwa hiyo ni jitahada nyingine ya nchi za magharibi kutaka kuipindua serikali na hivyo zinakwenda mbali zaidi ya azimio la Umoja wa Mataifa. Afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika amezituhumu nchi za Magharibi kuwa zinapuuza mpango wa amani wa umoja huo, ambao hautaji Gaddafi aondoke madarakani. Umoja wa Afrika umezihimiza pande zote kusitisha mapigano ili kuzuia vurugu zaidi. Hata operesheni za kijeshi zinazowalenga maafisa wa ngazi za juu wa Libya pamoja na miundo mbinu ya kijamii na kiuchumi zikomeshwe.

Libyan rebel fighters run across a street in the besieged city of Misrata, Libya, Saturday, April 23, 2011. Government troops retreated to the outskirts of Misrata under rebel fire Saturday and the opposition claimed victory after officials in Tripoli decided to pull back forces loyal to Moammar Gadhafi following nearly two months of laying siege to the western city. (AP Photo
Waasi wa Libya katika mji wa Misrata unaoshambuliwaPicha: AP

NATO haitaki kumuua Gaddafi

Siku ya Jumatatu, ndege za kijeshi ziliteketeza jengo mojawapo la Gaddafi. Maafisa wake wamesema hilo lilikuwa jaribio la kutaka kumuua. Lakini NATO inakanusha kwamba inataka kumuua. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Liam Fox, aliekutana na waziri mwenzake wa Marekani, Robert Gates, na wakuu wa majeshi ya nchi hizo mbili mjini Washington, aliwaambia maripota kuwa kwa maoni yao, vituo vyote vya uongozi na operesheni za kijeshi ni vituo halali vya kulengwa na baadhi ya vituo hivyo vimeshambuliwa.

Serikali ya Libya imeiomba Urusi kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kile kilichoitwa "jaribio la kumuua" Gaddafi pale ofisi yake ilipoteketezwa katika shambulio la Jumapili. Kwa maoni ya baadhi ya wachambuzi, vikosi vya magharibi sasa vinashambulia bila ya kufikia lengo la kijeshi.

Mwandishi: Martin,Prema/AFPE/DPAE/RTRE

Mhariri: Miraji Othman