1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea Syria licha ya jumuiya ya kiarabu kukubaliana kusitishwa kwa mapigano.

3 Novemba 2011

Licha ya serikali ya Syria kutangaza kukubali mpango wa jumuiya ya kiarabu kumaliza vita na kuleta amani nchini humo, majeshi huko yamesababisha vifo vya watu watatu katika mikoa kadhaa mjini Homs, Hama na Idlib.

https://p.dw.com/p/134Nv
Wawakilishi wa jumuiya ya kiarabu.Picha: picture-alliance/dpa

Hata baada ya serikali kutangaza kukubaliana na jumuiya ya kiarabu kumaliza vita nchini Syria, majeshi ya nchi hiyo yalishambulia mikoa kadhaa mjini Homs, Hama na Idlib. Hii imetokana na maandamano ya raia huko wanaotaka kuondoka mamlakani kwa rais wa sasa Bashar al Assad.

Katika eneo la Baba Amr linalopakana na mji wa Homs mtu mmoja ameuwawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa usalama.

Mwanaharakati mmoja raia wa Syria anayeishi nchini Lebanon, amesema majeshi pamoja na wafuasi wa rais Assad bado wanafanya visa vya kihuni mjini Homs, wakikamata na kuuwa watu licha ya jumuiya ya kiarabu kukubaliana kuwa majeshi yote na maafisa wa kijasusi waondolewe barabarani haraka iwezekanavyo.

Ägypten Kairo Arabische Liga Beratung über Syrien
Katibu mkuu wa jumuiya ya kiarabu Nabil AlarabiPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Hamad Bin Jassim, jana alitangaza umoja wa jumuiya ya kiarabu ulikubaliana kwa pamoja kusitisha mapigano nchini Syria, kuachiliwa huru kwa wale waliokamatwa tangu mageuzi kuanza nchini humo, kuondolewa kwa majeshi katika miji yote na mikoa ambapo kulikuwa na mapigano makali na kukubali jumuiya hiyo na waandishi wa habari wa taifa na kimataifa kuingia nchini humo na kuangalia mambo yanavyokwenda.

Bado haijakuwa wazi iwapo makubaliano haya ambayo yanatarajiwa kutekelezwa kati ya muda wa wiki mbili utaleta tofauti yoyote nchini Syria hasaa kwa wakati huu ambapo bado kuna visa vya ghasia na mauaji katika maeneo kadhaa nchini humo.

Hata hivyo raia nchini Syria sasa wamepanga maandamano makubwa zaidi ili kuipima serikali iwapo watatimiza ahadi yao ya kusitisha vita na kuleta amani Syria. Maandamano hayo hayajajulikana yatafanyika lini.

Kulingana na umoja wa mataifa zaidi ya watu elfu 3, wakiwemo watoto 187 wameuwawa, kufuatia oparesheni ya serikali dhidi ya waandamanaji wanaotaka demokrasia nchini humo yaliyoanza mwezi Machi mwaka huu.

Amina Abubakar AFP/AFPE

Mhariri Josephat Charo