1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea Syria licha ya makubaliano ya amani

29 Februari 2016

Mapigano yemeendelea kuripotiwa Syria kinyume na mpango wa amani uliofikiwa kwa ushawishi wa Marekani na Urusi. Saudi Arabia inatupa lawama kwa serikali ya Syria kutokuheshimu makubaliano.

https://p.dw.com/p/1I42H
Syrien Kafr Hamra Luftangriffe in Aleppo trotz Feuerpause
Picha: picture-alliance/abaca

Vikosi vya serikali ya Syria vimeidhibiti barabara muhimu inayoelekea katika mji wa kaskazini wa Aleppo baada ya kusonga mbele dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu IS hivi leo. Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia masuala ya haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London nchini Uingereza, mapambano makali yameendelea kati ya vikosi vya seriakli na wapiganaji wa kundi hilo katika eneo la kusini mashariki mwa mkoa wa Aleppo.

Ufanisi wa serikali ya Syria katika mkoa wa Aleppo kupitia msaada wa mashambulizi ya kutokea angani ya Urusi na wapiganaji washirika kutoka Iran na wa kundi la Hezbollah la Lebanon, unakuja katika siku ya tatu ya utekelezaji mkataba wa kusitisha uhasama kati ya Marekani na Urusi, ambao hauyajumuishi makundi ya Dola la Kiislamu na Al Nusra Front.

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Saudi Arabai, Adel al Jubeir, aliishutumu Urusi na serikali ya Syria kwa kukiuka usitishwaji mapigano nchini Syria. "Kuna uvunjifu wa usitishaji mapigano uliofanywa na vikosi vya Urusi na utawala wa Syria, na tunashauriana na nchi za kundi linaloisaidia Syria. Nadhani kujitolea kwa dhati kuuheshimu usitishwaji mapigano itakuwa ishara muhimu kutoka kwa utawala wa Syria."

Akizungumza katika mkutano na waandishiwa habari akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Denmark, Kristin Jensen, aliyekuwa ziarani mjini Riyadh, Jubeir alisema kutakuwa na mpango mbadala ikiwa itadhihirika wazi kwamba rais wa Syria, Bashar al Assad, na washirika wake hawayaheshimu makubaliano, lakini hakutoa maelezo yoyote.

Frank-Walter Steinmeier Porträt
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/B.v.Jutrczenka

Kwa upande wake waziri Jensen alitoa wito kuundwe muungano imara kuongeza shinikizo la kijeshi kwa utawala wa Assad kusaidia kuvimaliza vita nchini Syria. "Kuna suluhisho la kisiasa tu kwa tatizo la Syria, vita vya Syria, lakini suluhisho la kisiasa linaweza kupatikana kupitia kitisho cha kijeshi, vinginevyo Assad ataendelea na utawala wake wa kinyama ambapo amewaua maelfu ya raia wake mwenyewe na kuwafanya zaidi ya nusu ya wakazi kuwa wakimbizi."

Usitishwaji uhasama uambatane na mchakato wa kisiasa

Wakati haya yakiarifiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema usitishaji mapigano nchini Syria utaheshimiwa iwapo utaambatana na mchakato wa kisiasa. "Unaweza kuona katika sura za Wasyria wakati huu kwamba wasiwasi na matumaini vimekaribiana sana na bila shaka ni mapema mno kusema kama usitishwaji mapigano utadumu."

Steinmeier aliyasema hayo jana katika uwanja wa ndege wa Tegel mjini Berlin kabla kuondoka kwenda Marekani kwa mazungumzo zaidi na waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo, John Kerry.

Wizara ya mambo ya nchi za kigeni ya Urusi imesema leo kwamba Kerry alizungumza kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergei Lavrov, hapo jana kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya nchi zao kuhusu mpango wa kusitisha mapigano chini Syria.

Mwandishi: Josephat Charo/rtre/afpe/

Mhariri: Mohammed Khelef