1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaibuka upya Ukraine

Isaac Gamba
1 Februari 2017

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kusitishwa mapigano mara moja nchini Ukaraine ambako ghasia mpya zilizoibuka katika kipindi cha siku tatu zimeuwa watu 13.

https://p.dw.com/p/2WmOj
Ukraine Kämpfe in der Ostukraine in Awdijiwka | Essen
Picha: Getty Images/AFP/A. Filippov

Wito wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa umekuja baada ya vikosi vya Ukraine na waasi wanaoungwa mkono na Urusi kupambana katika siku ya tatu mfululizo katika mji wa Avdiivka.  Mji huo ulioko katika ukanda wa viwanda ulitumbukia tena katika hali ya mapigano baada ya waasi kuanzisha upya kampeni yao ya kurejesha maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Ukraine katika mapigano ambayo yamechukuwa karibu miaka mitatu sasa.

Mapigano hayo mapya yamegharimu maisha ya raia 13 na wapiganaji kutoka pande zote mbili tangu hapo jumapili ambayo yanaelezwa kuwa mabaya zaidi tangu pande zote mbili zilipokubaliana kusitisha mapigano Desemba 23mwaka jana.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alilazimika kukatiza ziara yake nchini Ujerumani  Jumatatu  na kuitisha kikao cha dharura cha baraza la ulinzi na usalama.

Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko Picha: REUTERS/M. Schlicht

Rais Poroshenko anahofu kuwa hatua ya kuchaguliwa Donald Trump kuwa Rais  wa Marekani inaweza kuzidisha mgogoro huo ambao ulianza muda mfupi tu baada ya kuondolewa madarakani kiongozi aliyekuwa akiiungwa mkono na Urusi mnamo mwaka 2014. Wasiwasi wake unatokana na msimamo wa Rais Trump kuendelea kumsifu mara kadhaa Rais Vladimir Putin. 

Msemaji wa Rais Putin Dmitry Peskov amesema serikali ya nchi hiyo inaaamini kuwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali ya sasa Ukraine  ndio chanzo cha mapigano hayo mapya.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP anasema alishuhudia wapiganaji wa kundi linalotaka kujitenga wakifanya mashambulizi makali kulenga mji huo ulio na idadi ya watu karibu 20,000.

Serikali yakiri tatizo la umeme

Msemaji wa jeshi la serikali ya Ukraine alisema hivi sasa wanakabiliwa na ukosefu wahuduma ya umeme na kuwa bado hawajatatua tatizo hilo hasa katika kipindi hiki cha msimu wa baridi kali.

Mtawala wa kijeshi wa mji huo Freedon Vekua alilieleza shirika la habari la AFP kuwa alikuwa akijiandaa kuwaondoa watu katika mji huo kutokana na hali hiyo ya baridi na pia kushindwa kupata ufumbuzi hadi sasa wa kurejeshwa kwa huduma ya umeme.

Ukraine hivi sasa inakabiliwa na hali  ya baridi kali ambapo kiwango cha joto kimeshuka hadi nyuzi 20 chini ya sufuri hivi sasa.

Shirika la ushirikiano na asalama barani ulaya OSCE linalohusika na kufuatilia ukiukwaji wa usitishaji mapigano  na pia kuratibu mazungumzo ya mani kati ya Urusi na Ukraine limesema mapigano hayo yaliyoibuka upya  yanaleta hofu hasa kutokana na idadi ya watoto 2,500  katika mji huo wanaoishi pasipo huduma ya maji na umeme.

Serikali ya Marekani imetoa mwito wa kusitishwa haraka mapigano hayo  ili kuepushaa mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo.

Mgogoro huo wa Ukraine hadi sasa umewaua kiasi ya watu 10,000 tangu ulipoibuka mnamo mwaka 2014.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri      : Gakuba Daniel