1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yamepamba moto nchini Yemen

21 Septemba 2011

Mapigano makali yameripuka leo mjini Sanaa licha ya mpango wa kuweka chini silaha ulioanza jana.Wimbi hili jipya la mapigano linahatarisha juhudi za kidiplomasia za kuumaliza mzozo wa Yemen

https://p.dw.com/p/12dw8
Waandamanaji waliojeruhiwa na polisi wa YemenPicha: dapd

Baada ya hali kuwa tulivu usiku kucha, milio ya risasi ikifuatiwa na mizinga ilihanikiza tangu asubuhi katika kitongoji cha eneo la kati la mji mkuu, Sanaa, inakokutikana pia nyumba ya makamo wa rais, Abd Rabbo Mansur Hadi.

"Hakuna anaeweza kutoka kuwashughulikia wahanga kutokana na jinsi mapigano yalivyopamba moto" amesema hayao mkaazi mmoja wa mtaa wa Ashrine, ambae kwa maoni yake pekee wanajeshi na askari kanzu ndio wanaopiga doria huku mapigano yakiendelea hadi wakati huu.

Duru za hospitali zinasema watu wasiopungua watano wanasemekana wamekufa leo. Jumla ya watu 75 wameuwawa tangu wimbi hili jipya la mapigano lilipozukla siku nne zilizopita.

Wakaazi wa mji mkuu wa Sanaa wanayaangalia kwa jicho la wasi wasi makubaliano ya kuweka chini silaha."Hali inatisha,mapigano yanaweza kuripuka wakati wowote" amesema Abdel Rahman, mtaalam wa kiufundi mwenye umri wa miaka 32 alipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa-AFP.

Jemen Protest Sicherheitskräfte
Maandamano ya wapinzani wa rais Ali Abdallah SalehPicha: dapd

Mazishi ya wahanga wa machafuko ya siku tatu zilizopita yalipangwa jioni hii katika uwanja wa mageuzi-kitovu cha maandamano ya mjini Sanaa dhidi ya rais Ali Abdallah Saleh.

Makubaliano ya kuweka chini silaha yalilengwa kurahisisha juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na umoja wa mataifa na Baraza la Ushirikiano la Ghuba kwa lengo la kuundwa serikali ya kipindi cha mpito nchini Yemen.

Duru za kidiplomasia zinasema makamo wa rais Abd Rabbo Mansour Hadi amepangiwa kukutana leo na mjumbe wa Umoja wa mataifa, Jamal Benomar, na mpatanishi wa Baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba Abdellatif al-Zayani. Wanadiplomasia hao wako Sanaa tangu jumatatu iliyopita wakiongoza juhudi za kuumaliza haraka mgogoro wa Yemen.

Massaker im Jemen September 2011
Mauwaji nchini YEmenPicha: picture alliance/dpa

Mapigano karibu na nyuma ya makamo huyo wa rais wa Yemen yanaweza kukorofisha mazungumzo hayo. Duru za kuaminika zinasema hata upande wa upinzani wa Yemen umeshindwa kuonana nao hapo jana.

Jana Marekani ilitoa mwito wa kupatikana "ufumbuzi wa kisiasa" ili kumaliza wimbi la matumizi ya nguvu nchini Yemen, nao Umoja wa Ulaya ukazungumzia haja ya kutiwa saini na kutekelezwa haraka mpango wa kuumaliza mgogoro huo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman