1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto Congo.

Ponda, Eric Kalume29 Oktoba 2008

Huku mapigano yakizidi kupamba moto katika eneo la mashariki mwa Jamahuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maelfu ya wakimbizi sasa wameanza kumiminika katika kambi ya wakimbizi ya Kibati, umbali wa kilomita 10 kutoka Goma.

https://p.dw.com/p/Fjml
Maelfu ya wakimbizi wahama makwao kukimbia vita Mashariki mwa Congo.Picha: AP


Hali hii ikiripotiwa, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa bado halijaafikiana kuhusu mpango wa kupelekwa wanajeshi zaidi wa kulinda amani katika eneo hilo linalokumbwa na vita.


Zaidi ya wakimbizi 3,000 wanaotoroka mapigano baina ya majeshi ya serikali ya Rais Joseph Kabila na waasi wa Laurent Nkunda katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameanza kuwasili katika mji huo wa Kibati karibu na mji wa Goma.


Akihutubia waandishi wa habari kutoka jimbo la Kivu kaskazini, kamanda wa kikosi cha jeshi hilo la Umoja wa Mataifa MONUC, Alan Doss, alisema kuwa wanajeshi wa kikosi hicho wametumia ndege aina ya Helkopta kuzima jaribio la kuuteka mji wa Goma.


Alisema kuwa jumla ya wanajeshi 6,000 wa jeshi hilo la MONUC, walitumiwa kuwafurusha wapiganaji hao wa muasi Laurent Nkunda ambao tayari walikuwa wameuzingira mji huo wa Goma.


Hata hivyo akiliarifu baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ilivyo katika eneo hilo la Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, mkuu wa kikosi hicho cha kuhifadhi amani nchini humo Allan Le Roy, alitaja hali ilivyo katika eneo hilo kuwa mbaya, huku waasi wa Laurent Nkunda wakikaribia kuuteka mji huo ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini.


Lakini baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa, yaripotiwa halijaafikiana kuhusu ombi la kupelekwa kwa wanajeshi zaidi wa kikosi cha MONUC, kusaidia juhudi za kulinda amani katika eneo hilo la mashariki mwa Kongo.

Mapema wiki hii, rais Jospeh Kabila alitoa ombi kwa baraza hilo la usalama kuongeza idadi ya wanajeshi wa kikosi cha MONUC, kusaidia juhudi za jeshi la serikali yake kupambana na waasi hao wa Laurent Nkunda, ingawa wakati wa kikao chake, baraza hilo lilielezea tu kusikitishwa kwake na kuendelea kwa mapigano katika eneo hilo.


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anayehudhuria kikao cha Umoja huo kuhusu suala la wakimbizi, kinachofanyika mjini Manila, alisema kuwa amesikitishwa na mapigano hayo, ingawa hakuzungumzia suala la kupelekwa kwa wanajeshi zaidi katika eneo hilo la Mashariki mwa Kongo.


Wakati huo huo kamishna mkuu wa shirika la misaada la umoja wa Ulaya Loius Michel, ambaye ameanza ziara yake ya siku mbili nchini humo, amesema kuwa atajaribu kutumia fursa hiyo kuzihimiza pande zinazozozana kusitisha mapigano hayo.



Waasi wa Laurent Nkunda wamezidisha mapigano nchini humo tangu mwezi Agosti dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila kufuatia kuvunjika kwa mkataba wa amani.