1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto magharibi mwa Cote d'Ivoire

7 Machi 2011

Wapiganaji wanaomuunga mkono Alassane Ouatarra wameuteka mji mmoja wa upande wa magharibi uliokuwa ukidhibitiwa na wafuasi wa mpizani wake mkuu, Laurent Gbagbo

https://p.dw.com/p/10UVp
Machafuko nchini Cote d'IvoirePicha: picture alliance / dpa

Mapigano makali yalitokea usiku wa kuamkia leo kati ya wafuasi wanaomuunga mkono Laurent Gbagbo na waasi wanaomuunga mkono hasimu wake, Alassane Ouatarra. Wafuasi hao wa Ouatarra waliuteka mji wa Toulepleu ulioko eneo la mpaka wa Cote d'Ivoire na Liberia.

Duru za kijeshi zinaeleza kuwa milio ya risasi ilisikika na inaaminika kuwa silaha nzito zilitumiwa. Itakumbukwa kuwa mwaka 2002 hadi 2003, mji huo wa Toulepleu uligubikwa na mapigano makali wakati waasi walipopambana na wapiganaji wa Laurent Gbagbo. Hali ni ya wasiwasi kama alivyofahamisha mkaazi wa eneo hilo.

Elfenbeinküste Präsident Laurent Gbagbo
Rais wa Cote d'Ivoire, Laurent GbagboPicha: AP

Milio ya risasi ilisikika pia katika mtaa wa Abobo ulioko mjini Abidjan. Itakumbukwa kuwa wanawake saba waliuawa mtaani humo kwenye maandamano yaliyotokea siku chache zilizopita. Kulingana na msemaji wa Kamishna wa Masuala ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Rupert Colville, wahuni wanawazuwia baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuondoka.

"Tumepokea taarifa zinazoeleza kuwa kundi moja la wahuni ambalo halijulikani, wanaojiita Abobo Commandoes, wanawazuia watu kutoka mtaa wa Abobo na mitaa miengine. Wahuni hao wanawatumia wakazi kama ngao katika mapambano kati yao na wanajeshi wanaomuunga mkono Laurent Gbagbo."

Mapigano hayo mapya yamewafanya wakazi wengi wakimbilie nchi jirani ya Liberia ambako maelfu wamekuwa wakipata hifadhi tangu mgogoro huo wa kisiasa kuanza miezi mitatu iliyopita. Hali hiyo imeufanya Umoja wa Mataifa kutahadharisha kuwa huenda vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka Cote d'Ivoire.

Alassane Ouattara
Alassane Ouattara, anayetambuliwa kimataifa kama mshindi halali wa urais Cote d'IvoirePicha: AP

Kikao cha Umoja wa Afrika

Kwa upande mwengine, Umoja wa Afrika unasubiri kauli ya Gbagbo baada ya kumualika rasmi pamoja na mpinzani wake Ouatarra kukaa kwenye meza ya mazungumzo mjini Addis Ababa. Ili kuzipa msukumo juhudi za kidiplomasia za kuusuluhisha mgogoro huo wa kisiasa, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, aliizuru Cote d'Ivoire mwishoni mwa wiki alikokutana na wanasiasa hao wanaohasimiana.

Kikao hicho kilichopangwa kufanyika siku ya Alhamisi kitawaleta pamoja wanasiasa hao na jopo maalumu la marais wa mataifa matano wanaoushughulikia mzozo huo.

Siku ya Jumamosi, Alassane Ouatarra aliripotiwa kusema kuwa atakihudhuria kikao hicho. Mpaka sasa haijabainika iwapo Laurent Gbagbo au raisi wa baraza la masuala ya katiba, Paul Yao N'Dre aliye na uhusiano wa karibu naye, watauhudhuria mkutano huo.

Cote d'Ivoire inakabiliwa na mkwamo wa kisiasa ulioanza baada ya uchaguzi wa mwezi wa Novemba mwaka uliopita kuzua utata. Wanasiasa hao wawili wote wanadai kuwa washindi wa uchaguzi huo.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo