1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto Ukraine

Mjahida2 Februari 2015

Mapigano makali yameripotiwa kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaoiunga mkono Urusi wanaong'ang'ania udhibiti wa eneo muhimu la usafiri la Debaltseve.

https://p.dw.com/p/1EUL1
Waasi wa Ukraine wakiwa ndani ya gari la kivita Mashariki mwa nchi hiyo
Waasi wa Ukraine wakiwa ndani ya gari la kivita Mashariki mwa nchi hiyoPicha: REUTERS/Maxim Shemetov

Milio ya mabomu ilisikika karibu na mji unaodhibitiwa na serikali ya Ukraine wa Debaltseve, mji uliomuhimu na ulio karibu na miji miwili ya Donetsk na Luhansk, inayodhibitiwa na waasi wanaoiunga mkono Urusi. Waasi kwa sasa wanajaribu kuwazunguka wanajeshi wa serikali ya Ukraine walioko mjini Debaltseve.

Kulingana na Kamanda wa polisi katika eneo hilo Yevgen Lukhaniv baadhi ya watu wanaendelea kuukimbia mji huo, wengi wakilalamika juu ya ukosefu wa maji na hata umeme. Hata hivyo msemaji wa jeshi la serikali Volodymyr Polyovyi amesema bado mapigano yanaendelea na kuahidi kwamba serikali haitoachia eneo hilo kutwaliwa na waasi.

Mapigano hayo yanatokea wakati Marekani pamoja na kamanda wa Jumuiya ya kujihami NATO, wakitarajia kutoa silaha kwa wanajeshi wa serikali ya Ukraine. Aidha gazeti moja la Marekani New York Times, lililoripoti hayo hapo jana limeandika kwamba, Utawala wa rais Barrack Obama unafikiria kutoa msaada wa vifaa vya kijeshi au msaada ambao sio wa kijeshi kama vifaa vya kujikinga na mashambulizi pamoja na vifaa vya matibabu ambayo tayari inatoa kwa Ukraine.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: picture-alliance/dpa/M.Lazarenko

Kwengineko Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry anatarajiwa kuelekea Ukraine hapo kesho kwa mazungumzo na rais Petro Poroshenko na maafisa wengine wakuu wa serikali ya Ukraine. Wiki iliopita Rais Obama alielezea wasiwasi wake juu ya mapigano mapya kati ya vikosi vya serikali na waasi huku akisema Marekani inaangalia mbinu zote kuisaidia Ukraine.

Urusi yalaumiwa kwa mgogoro wa Ukraine

Serikali za Magharibi na Ukraine wamekuwa wakiishutumu Urusi kwa kutuma wanajeshi pamoja na silaha kwa waasi wa Mashariki mwa Ukraine hatua ilioonekana kama ya kuwaimarisha waasi hao na kuchochea mashambulizi zaidi. Madai ambayo Urusi inaendelea kuyakanusha.

Wakati huo huo waasi hao wanasemekana kuwa na silaha nzito na vifaa vyengine vya kijeshi wanaodai kupata kutoka kwa wanajeshi wa Ukraine waliokuwa wanakimbia mapigano. Kwa upande mwengine tangu kluanza kwa mapigano mwezi wa Aprili mwaka uliopita watu takriban 5,100 wameripotiwa kuuwawa.

Siku ya Jumapili jeshi la Ukraine lilisema wanajeshi 13 wameuwawa huku wengine 20 wakijeruhiwa ndani ya saa 24. Hali hiyo imeongeza idadi ya wanajeshi waliofariki kutokana na mapigano ya siku mbili kufikia watu 28. Maafisa wengine wa serikali na maafisa wa waasi wameongeza kuwa, raia 17 waliuwawa katika mapigano hayo Mahsriki mwa Ukraine.

Baadhi ya wawakilishi wa pande zinazohasimiana walipokutana mjini Minsk
Picha: picture-alliance/dpa

Mgogoro nchini Ukraine unazidi kupanuka huku pande zinazohasimiana zikijaribu kutafuta njia ya kukubaliana juu ya amani ya nchi hiyo katika mazungumzo yalioshindwa siku ya Jumamosi.

Wakizungumza kwa njia ya simu rais wa Ufaransa Francois Hollande, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ukraine Petro Poroshenkowalielezea masikitiko yao juu ya kusambaratika kwa juhudi hizo katika mji mkuu wa Belarus, Minsk.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu