1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka tena Rutshuru kati ya M23 na Mai Mai

12 Julai 2023

Mapigano makali yameshuhudiwa tena kati ya waasi wa M23 na kundi la vijana wa Maimai wanaojiita Wazalendo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

https://p.dw.com/p/4TlHe
Mai-Mai Milizen im Kongo
Picha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Isaac KIBIRA, mjumbe wa gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini katika eneo la Bwito, ameiambia DW kwamba waasi hao wa M23 walizilenga ngome za vijana hao wajiitao wazalendo katika kijiji cha Bukombo wilayani Rutshuru karibuni kilometa 19 kutoka mji wa kimkakati wa Kitshanga, ambako milio ya silaha ilirindima mchana kutwa wa jana Jumanne.

Soma pia: Mapigano yazuka upya kati ya waasi wa M23 na vijana wazalendo

Afisa huyu wa serikali aliye mafichoni amebainisha pia kuwa mamia wa raia wengine wameendelea kukimbia nyumba zao kufuatia hali ya wasiwasi inayoshuhudiwa katika eneo hilo linalolengwa sasa na mashambulizi hayo ya waasi hao wa M23  wanaoshukiwa kusaidiwa na nchi jirani ya Rwanda.

Maoni ya wakaazi wa Goma juu ya vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Hayo yakijiri, mjumbe maalum wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye mzozo wa mashariki mwa Kongo, Rais wa zamani wa Kenya UHURU KENYATA pamoja na maafisa wengine wa serikali ya Kongo wanasubiriwa hii leo katika mji huu wa Goma ambako watatathmini mwenendo wa mchakato wa amani eneo hili la mashariki ambako makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 bado yanatiliwa shaka.

Hili ni eneo lilikotumwa kikosi cha walinda amani cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambacho kinakosolewa vikali na baadhi ya raia:

Waziri wa Ulinzi Jean PIERRE BEMBA na mwenzake wa Ushirikiano wa Kikanda, Mbusa Nyamwisi, watashiriki mkutano huo ambayo ajenda kuu ni pamoja na kukusanywa kwa waasi wa M23 katika kambi ya Rumangabo kama ilivyotakiwa awali na viongozi wa kikanda.

Hadi sasa waasi wa M23 hawajatowa ahadi yoyote ile kwa usitishwaji wa mapigano yanayoendelea katika wilaya za Masisi na Rutshuru.