1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka upya Chad

27 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CTht

NDJAMENA.Kumeibuka mapigano makali kati ya waasi na majeshi ya Serikali, huko kusini mwa Chad.

Mapigano hayo yametokea kiasi cha kilomita 40 kutoka eneo la Darfur kwenye mpaka na Sudan eneo ambalo kiasi cha askari 4,000 wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kupelekwa kulinda usalama.

Jeshi la Serikali ya Chad limesema kuwa katika mapigano hayo limefanikiwa kuwaua mamia kadhaa ya waasi na kuharibu magari kadhaa.

Jeshi hilo limesema kuwa miongoni mwa waliyouawa ni pamoja na maafisa wa juu wa jeshi la waasi, General Dirmi Haroun na Kanali Guende Abdramane.

Lakini kwa upande wao waasi hao wamedai kuwa wapiganaji wake 17 wameuawa na wamefanikiwa kuwauawa askari zaidi ya mia moja wa serikali.

Kuzuka kwa mapigano hayo kumemaliza miezi kadhaa ya hali ya utulivu kutokana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Libya.