1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano zaidi Syria

MjahidA6 Novemba 2012

Nchini Syria bomu moja lililoegeshwa ndani ya gari liliripuka na kuutikisa mji wa Damascus mapema leo asubuhi

https://p.dw.com/p/16dSe
Moja ya mashambulizi mjini Damascus
Moja ya mashambulizi mjini DamascusPicha: AFP/Getty Images

Hii ni kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu nchini humo. Shambulizi hili hata hivyo limetokea siku moja tu baada ya watu takriban 250 kuuwawa, katika mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu kushindwa usimamishaji mapigano mwezi uliopita.

Kulingana na shirika hilo la kutetea haki za binaadamu, bomu hilo lililoripuka katika mji ulio karibu sana na mji mkuu Damascus, lilisababisha majeruhi kadhaa pamoja na uharibifu mkubwa.

Mashambulizi ya angani yalilenga pia mji wa Douma ulioko kilomita 13 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Damascus ambapo mabomu mawili yalirushwa katika jengo moja huku makombora yakiangushwa katika eneo la Al Bab katikati mwa mji wa Homs.

Kifaru cha jeshi la Israel
Kifaru cha jeshi la IsraelPicha: dpad

Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu lenye makao yake makuu mjini London limeongeza kusema kuwa vikosi vya serikali vimeendelea kushambulia maneo mengine ya magharibi mwa eneo la Takia mjini Homs na Quneitra mahali ambapo jeshi la Israel lilisema siku ya Jumatatu kuwa jeshi la Syria lilishambulia gari lake la kijeshi.

Awali ilisemekana kuwa watu takriban 247 waliuwawa katika mapigano ya hapo jana wakiwemo wanajeshi 93, raia 86 na waasi 68.

Hata hivyo katika moja ya visa vibaya zaidi kwa upande wa vikosi vya Bashar Al Assad tangu kuanza kwa mapigano miezi 20 iliopita, ni pale gari moja la waasi lililowekwa mabomu liliporipuka na kusababisha vifo vya majeshi 50 katika kambi moja ya kijeshi katika mkoa wa Hama hapo jana. Tangu kuanza kwa mapigano hayo takriban watu 36,000 wameuwawa nchini Syria huku wengine wengi wakipoteza makaazi yao.

Wapinzani Syria wakutana Alhamisi mjini Doha

Wapinzani nchini Syria
Wapinzani nchini SyriaPicha: Reuters

Huku hayo yakiarifiwa makundi kadhaa ya upinzani nchini Syria yanajitayarisha kufanya mkutano wao siku ya Alkhamisi wiki hii. Mkutano ambao ni wa kuonesha umoja wao ili kupata kuungwa mkono na jamii ya kimataifa na pia kutarajia kuwa huenda wakapewa silaha za kupambana na vikosi vya serikali ya Bashar Al Assad.

Mkutano huo wa Alhamisi utazungumzia pia pendekezo la kiongozi wa upinzani Riad Seif kuunda kundi la raia 50 ambao baadaye wataunda serikali ya muda na kushirikiana na jeshi la waasi jambo ambalo ni muhimu katika kupata uungaji mkono wa jamii ya Kimataifa.

Mwandishi: Amina Abubakar/ AFP/ Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman