1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapinduzi ya kijeshi Mauritania

6 Agosti 2008

Rais Ould Cheikh Abdillahi, waziri mkuu na waziri wake wa ndani watiwa nguvuni.

https://p.dw.com/p/Ere5
Eneo moja la usafiri wa umma katika mji mkuu Noakchott .Picha: AP

Tangazo fupi katika televisheni ya taifa lilisema rais Sidi Mohamed Ould Cheikh Abdallahi amepinduliwa na kile kilichotajwa kuwa ni baraza la taifa, litaongozwa na mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais Jenerali Mohamed Ould Abdel Aziz na kwamba Bw Abdallahi sasas ni "rais wa zamani." Hakuna maelezo zaidi yaliotolewa.

Taarifa zinasema maafisa waliofanya mapinduzi hayo walimtia nguvuni Rais,Waziri wake mkuu na waziri wa ndani.

tangu mapema asubuhi aya leo redio na televisheni ya taifa mjini Nouakchott zilisitisha matangazo yote . mapinduzi hayo yamefanyika baada ya rais huyo kuwafukuza kazi maafisa wanne wa kijeshi wa ngazi ya juu.

Binti wa rais Abdallahi, Amal Mint Cheikh Abdallahi alisema maafisa wa usalama wa kikosi cha ulinzi wa rais waliingia Ikulu mapema asubuhi na kumkata rais huyo na sasa akiwa pamoja na waziri mkuu na waziri wa ulinzi wamepelekwa mahala pasipojulikana.

Alisema wamo familia ya kiongozi huyo bado wamezuiliwa Ikulu na kwamba wanajeshi walikua kila mahala ndani ya jengo hilo wakiwa na silaha .

Abdallahi alishinda uchaguzi wa rais mwaka jana na kumchukua madaraka kutoka utawala wa kijeshi uzliokua madarakani tangu alipoangushwa Rais Maaouya Ould Sidi Ahmed Taya katika mapinduzi yasiomwaga damu 2005.

Mwezi Mei mwaka huu, alifanya mageuzi ya baraza la mawaziri baada ya serikali kukosolewa jinsi inavyolishughulikia tatizo la kuongezeka mno kwa bei ya vyakula na pia kuhusiana na hujuma zilizofanywa mwaka jana na wale wanaojiita , jeshi la al-Qaeda katika Afrika kaskazini.

Serikali mpya ikaundwa bila ya vyama vya upinazani kile cha umoja kwa ajili ya maendeleo UFP na cha Waislamu -Tawassoul , ambavyo vilikuwemo katika serikali ya awali.

Matukio ya leo pia yanafuatia kujitoa katika kikao cha bunge juma hili kwa wanachama wengi wa chama tawala cha Rais Abdullahi, katika kile kinachotajwa na baadhi ya duru za kisiasa kwamba ni kitendo kilichoungwa mkono na maafisa wa kijeshi.

Mauritania imekumbwa na mlolongo wa mapinduzi tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa 1960. Mapinduzi ya kwanza yalimuangusha rais wa kwanza Mokhtar Ould Dadah 1978 na mwanajeshi Mohamed Ould Haidallah kutangazwa rais. Haidallah alipinduliwa na Maaouya Sid Ahmed Taya 1984 ambaye aliangushwa na Kanali Ely Ould Mohamed Vall 2005 wakati akihudhuria mazishi ya Mfalme Fahd wa Saudi Arabia.

Jenerali Vall aliyeahidi tangu awali kwamba atamaliza udikteta na kuitisha uchaguzi wa kidemokrasi, alitekeleza hadi hiyo na kukabidhi madaraka kwa rais aliyechaguliwa kidemokrasi baada ya uchaguzi wa Machi 2007.

Umoja wa Afrika ambao msimamo wake ni kutotambua utwaaji madaraka kwa nguvu, umejiunga na Umoja wa mataifa na Umoja wa ulaya kulaani mapinduzi hayo.