1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marais wa Afghanistan na Pakistan wakutana Uturuki.

Halima Nyanza25 Januari 2010

Marais wa Pakistan na Afghanistan wanakutana leo mjini Istanbul, katika mazungumzo juu ya usalama, yanayofadhiliwa na Uturuki, kujadili ushirikiano wao dhidi ya wapiganaji wa Al Qaeda.

https://p.dw.com/p/LgS4
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan (kulia) na Rais wa Uturuki Abdullah Gul wamekutana kuzungumzia hali ya Afghanistan.Picha: AP

Mkutano huo kati ya Rais Hamid Karzai wa Afghanistan na mwenziye wa Pakistan, Asif Ali Zardari, unakuja siku chache tu kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa, utakaofanyika London, Uingereza, wenye lengo la kuhamasisha maendeleo ya Afghanistan.

Rais wa Uturuki Abdullah Gul, ndio mwenyeji wa mkutano wa Istanbul, ambao pia utahudhuriwa na Wakuu wa majeshi na vyombo vya Usalama vya Afghanistan na Pakistan.

Tayari Rais Gul amekutana kwa mazungumzo na Rais Karzai, ambaye yuko mjini Istanbul kama kituo chake cha kwanza katika kutafuta kuungwa mkono na msaada wa fedha kwa ajili ya serikali yake, kabla ya kuelekea Berlin, Ujerumani na baadaye Uingereza.

Viongozi hao wamekutana mapema leo na kwamba Rais Gul atafanya pia mazungumzo na Rais wa Pakistan Asif Zardari kabla ya viongozi hao watatu kufungua mkutano huo.

Rais Gul kesho pia atakuwa mwenyeji wa mkutano utakaozijumuisha nchi jirani na Afghanistan, kuzungumzia njia za kuisaidia nchi hiyo iliyokumbwa na vita, kujiimarisha.

Mkutano huo utakao hudhuriwa na Marais wa Afghanistan na Pakistan, utawashirikisha pia maafisa waandamizi kutoka Iran, China, Tajikistan na Turkmenistan pamoja na wawakilishi kutoka nchi kadhaa na jumuia za kimataifa, ambapo Uingereza itawakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje, David Miliband.

Mkutano huo wa kesho una madhumuni ya kuzihimiza nchi kushughulikia matatizo ya kanda yao, kuliko kuziachia zaidi nchi za magharibi na pia kusisitizia haja ya kuunga mkono juhudi za kijeshi dhidi ya Taliban kwa hatua za kiuchumi na kijamii.

Uhusiano kati ya Kabul na Islamabad umekuwa wa mashaka, wakati ambao majimbo ya kaskazini magharibi mwa Pakistan yamekuwa ngome ya watu wenye misimamo mikali ambao wameikimbia Afghanistan, baada ya uvamizi uliofanywa na Marekani kuung'oa utawala wa Taliban mwishoni mwa mwaka 2001.

Mkutano wa Istanbul ni wa nne kufanyika katika mazungumzo ya kutengeneza mambo, tangu mwaka 2007, chini ya usimamizi wa Uturuki, nchi pekee ya kiislamu iliyo mwanachama katika Jumuiya Kujihami ya NATO.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, ap)

Mhariri: Miraji Othman