1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden na Xi kukutana pembezoni mwa mkutano wa APEC

Zainab Aziz
15 Novemba 2023

Marais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi Jinping wanajiandaa kufanya mkutano muhimu unaotarajiwa kuleta utulivu kwenye mahusiano kati ya mataifa hayo mawili makubwa.

https://p.dw.com/p/4YpGS
Indonesien Bali G20-Gipfel | Treffen Xi Jinping, Präsident China & Joe Biden, Präsident USA
Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Rais wa Marekani amejiweka tayari kukabiliana na mwenzake wa China katika maswala magumu yakiwemo ya biashara, uhusiano unaochipuka kati ya China na Iran na vilevile masuala yanayohusiana na haki za binadamu.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Andrew Harnik/AP/dpa/picture alliance

Viongozi hao wawili, watakutana kando mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Asia na Pasifik (APEC) unaofanyika mjini California.

Kulingana na maafisa wa utawala wa Marekani, Biden na Xi watafanya mazungumzo yao ya ana kwa ana katika nyumba ya mashambani ambayo pia ni nyumba ya makumbusho ya Filoli Estate, iliyoko takriban kilomita 40 kusini mwa San Francisco.

Hata hivyo kutokana na sababu za kiusalama ikulu ya Marekani na serikali ya China bado hazijathibitisha kuwa eneo hilo ndiko hasa Biden na Xi watapokutana.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Kyodo/picture alliance

Marais hao wa Marekani na China walizungumza mara ya mwisho mwaka mmoja uliopita na tangu wakati huo, uhusiano wa mataifa hayo mawili makubwa kiuchumi umedorora na hasa baada kudunguliwa puto la kijasusi la China lililokuwa limepitia kwenye anga ya Marekani na pia juu ya tofauti ya Marekani na China kuhusiana na kisiwa kinachojitawala cha Taiwan, vilevile juu ya udhibiti wa usafirishaji nje bidhaa za nchi hizo napia kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati na ya barani Ulaya.

Mengine ni kuhusu udukuzi wa China wa barua pepe za afisa wa rais Biden miongoni mwa matukio mengine.

Msemaji wa Baraza la Kitaifa la ikulu ya Marekani John Kirby
Msemaji wa Baraza la Kitaifa la ikulu ya Marekani John KirbyPicha: Bonnie Cash/UPI Photo/newscom/picture alliance

Msemaji wa Baraza la Kitaifa la ikulu ya Marekani John Kirby amesema rais Joe Biden hataogopa kumkabili Xi Jinping mahala ambapo makabiliano yanahitajika katika masuala ambayo Marekani na China hazikubaliani. 

Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning, amesema jambo la muhimu kati ya Marekani na China ni kufanya kazi kwa pamoja:

Msemaji wa Baraza la Kitaifa la ikulu ya Marekani John Kirby amesema rais Biden atajikita katika kudhibiti ushindani wa kiuchumi unaozidi kuwa mkali kati ya Marekani na China na wakati huo huo anataka kuweka njia wazi za mawasiliano ili kuzuia kutokuelewana kati ya mataifa hayo mawili hali ambayo inaweza kusababisha migogoro ya moja kwa moja kati ya nchi hizo zenye nguvu.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao NingPicha: Andy Wong/AP Photo/picture alliance

Biden anatarajiwa kutetea hatua ya Marekani ya kudhibiti mauzo ya nje ya chipu za kielektroniki Lakini pia atamhakikishia Xi Jinping kwamba Marekani haitaki vita vya kiuchumi na Beijing.

Xi, kwa upande wake anatafuta uhakikisho kutoka kwa Biden kwamba Marekani haitaunga mkono uhuru wa Taiwan na haitaanza vita mpya baridi au kuukandamiza ukuaji wa uchumi wa China.

Urusi imesema mkutano wa viongozi wa Marekani na China ni wa manufaa kwa ulimwengu mzima.

Vyanzo: AP/AFP