1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marais wa zamani kadhaa barani Afrika waingilia mzozo wa Kenya

Siraj Kalyango8 Januari 2008

Wajaribu kuleta maridhiano ya kitaifa

https://p.dw.com/p/CmSV
Joaquim Chissano,rais wa zamani wa Msumbiji ni miongoni mwa marais wa zamani wa baadhi ya nchi za Afrika ambao wanajaribu kupatanisha pande mbili husika nchini Kenya.Wengine ni Benjamin Mkapa wa Tanzania,Masire wa Botswana na Kaunda wa Zambia.Picha: AP

Viongozi kadhaa wa zamani barani Afrika wawasili Kenya katika juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa na kikabila uliotokea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi Disemba 2007.

Matokeo hayo yalimpa ushindi rais Mwai Kibaki hatua ambayo inapingwa na mpinazani wake Mkuu Raila Odinga.Pingamizi hizo zilizusha ghasia na fujo ambapo watu wasiopungua 400 kupoteza maisha yao.

Marais wa zamani wa baadhi ya nchi za kiafrika nao wameingia katika mchakamchka wa kutafuta suluhu kwa matatizo ya kisiasa yanayoikumba Kenya kwa sasa.

Miongoni mwa hao ni Benjamin Mkapa wa Tanzania, Joachim Chissano wa Msumbiji,Katumile Masire wa Botswana na Kenneth Kaunda wa Zambia.

Serikali ya Kenya inasema viongozi hao wa zamani wataungana na mweyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika-John Kufour-rais wa sasa wa Ghana.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Kenya ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mbali na kukutana na rais Kibaki pamoja na washika dau wengine kuhusiana na mgogoro huo pia watakutana kwa mazungumzo na rais wa zamani wa Kenya –Daniel Arap Moi.

Afisa wa serikali amesema kuwa miongoni na mengine majadiliano yanahusu jinsi ya kuleta utulivu na maridhiano ya kitaifa nchini humo kufuatia ghasia za kisiasa na kikabila zilizoikumba Kenya punde tu baada ya kumalizika kwa uchaguzi mwezi disemba mwaka 2007.

Matokeo ya uchaguzi wa Disemba 27, yalimrejesha madarakani rais Mwai Kibaki.Lakini mpinzani wake Raila Odinga alipinga hiyo na wachunguzi wengi kuonyesha wasiwasi na jinsi kura zilivyohesabiwa.Na mjumbe maalum wa Marekani Afrika asema kuwa hicho kikiwa ndio kitovu cha mgogoro huo-huenda kulitokea mizengwe na pande zote mbili zaweza kuwa zilihusika kwa njia moja au nyingine.

WaKenya wengi wanasema kutoaminina kulioko kati ya rais Kibaki na mpinazani wake Raila Odinga ndio mkingamo wa kupatikana kwa suluhu.

Rais Kibaki kwa upande wake amesema yuko tayari kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.Lakini Odinga namtaka ajiuzulu na pia ametoa masharti ya kukaa nae kwa meza moja.

Rais John Kufour anatarajiwa kufanya mazungumzo pia na Bw Odinga.

Kufour aliwahi kuhusika katika juhudi za kutua migogoro nchini Liberia na Ivory Coast.

Pia juhudi zingine zimefanywa wiki iliopita na mshindi wa tuzo ya Nobel Askofu desmond tutu wa Afrika kusini pamoja na mjumbe wa juu wa Marekani barani Afrika Jendayi Frazer.

Juhudi hizo zote zinafanywa kutokana na athari za kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa disemba.Watu wengi walipoteza maisha yao katika ghasia zilizofuata.Takwim mpya zinaonyesha kuwa sasa waliofariki wanafikia 600, na walioachwa bila makazi wanafikia laki mbili unusu.