1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani imewatambua waasi Libya

16 Julai 2011

Marekani imejiunga na mataifa mengine makuu yenye nguvu duniani katika kulitambua baraza la kitaifa la waasi nchini Libya kuwa taasisi halali ya uongozi nchini humo.

https://p.dw.com/p/11wU8
Mkutano wa kundi la mashauriano kuhusu Libya, mjini Istanbul UturukiPicha: dapd

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton alitangaza hayo katika mkutano mjini Istanbul Uturuki, wa zaidi ya mataifa 30 na taasisi za kimataifa, zijulikanazo kama kundi la mashauriano kuhusu Libya. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema kundi hilo liliahidi kuwaunga mkono waasi hao katika jitihada zao za kutaka kumuondoa uongozini Muammer Gaddafi.

Hillary Clinton Washington Pressekonferenz
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary clintonPicha: dapd

Kutambuliwa baraza hilo la waasi huenda kukasababisha kutolewa fedha nyingi. Uturuki imesema dola bilioni 3 za mali ya Libya zilizozuiliwa zitatolewa , ili muradi fedha hizo zitumike kwa sababu za kibinadamu pekee. Makubaliano ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa pamoja na vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala wa Gaddafi, vimezuia fedha za Libya katika nchi za nje. Gaddafi anakataa kujiuzulu na amesema atapigana hadi mwisho.

Mwandishi: Maryam Abdalla,AFP, dpa, Reuters
Mhariri: Kitojo,Sekione