1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani inahitaji uongozi bora zaidi - Zeid al-Hussein

Mohammed Khelef
8 Machi 2017

Mkuu wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa amemkosoa vikali Rais Donald Trump wa Marekani kuwa kushindwa kukabiliana na kuenea kwa chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa kidini unaosambaa kwa kasi.

https://p.dw.com/p/2YqQv
Schweiz UN-Menschenrechtsrat Said Raad al-Hussein
Picha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

Zeid Ra'ad al-Hussein  amewaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba ana wasiwasi sana na jinsi wimbi la ubaguzi linavyozidi kuwa kubwa, chuki dhidi ya Mayahudi, na mashambulizi dhidi ya walio wachache kidini na kijamii.

Akionekana mwenye hasira, kamishna huyo mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa ameionya serikali ya Marekani dhidi ya kuwageuza Waislamu na Wamexico wote kuwa wahalifu, na pia dhidi ya madai ya uongo juu ya kiwango kikubwa cha uhalifu miongoni mwa wahamiaji, zenye lengo la kuchochea mtazamo mbaya dhidi ya wageni, na ambao unatumika sasa kuwahukumu wageni hao.

"Mambo haya yanatishia kuongeza utumiaji wa mahabusu dhidi ya watu, wakiwemo watoto. Kuwahamisha watu kwa lazima ni sawa sawa na adhabu ya jumla jamala na kuvunja sheria za kimataifa, ikiwa kutafanyika bila ya utaratibu wa kisheria. Ninawatiwa wasiwasi sana na mabadiliko haya ambayo yanawakabili watoto wanaowekwa vizuizini, au wanaoweza kuziona familia zao zikisambaratishwa," alisema Zeid.

USA Donald Trump vor dem US-Kongress in Washington
Donald Trump anatuhumiwa kuchangia kwenye wimbi jipya la chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa kidini nchini Marekani.Picha: Reuters/J. Lo Scalzo

Akimlenga moja kwa moja Trump, Zeid alisema anafadhaishwa na majaribio ya rais huyo wa Marekani kuwatisha au kuwahujumu waandishi wa habari na majaji. Kauli yake hii inaakisika na shutuma walizonazo vyombo vikubwa vya habari na pia wanaharakati wa uhuru wa kujieleza dhidi ya Trump wanayesema anaidhalilisha tasnia yao, ikiwemo kuviita vyombo vya habari kuwa ni "adui wa umma."

Marekani ni mjumbe wa baraza hilo lenye wajumbe 47 na ilikuwa mwanachama mwenye ushawishi mkubwa katika kipindi chote cha miaka minane cha Rais Barack Obama. Lakini akiuwakilisha utawala wa Trump kwenye baraza hilo wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Erin Barclay, alisema kazi zinazofanywa na baraza hilo zinakwendana kinyume na misingi ya Marekani, hasa ukosowaji wa baraza dhidi ya Israel.

Akizungumzia mateso ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar, Zeid alisema dhuluma dhidi yao inalingana na "uhalifu dhidi ya ubinaadamu", ambapo ripoti zilizokusanywa na baraza la haki za binaadamu kwenye makambi ya wakimbizi nchini Bangladesha zinathibitisha "kiwango kikubwa cha mateso na mauaji ya maangamizi."

Akizungumzia vita dhidi ya madawa ya kulevya vinavyoongozwa na Rais Rodrigo Duterte nchini Ufilipino, Zeid alitaka kuwepo kwa uchunguzi kina na huru juu ya mauaji yanayofanywa na serikali, wito ambao pia ameutoa kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alikotaka uchunguzi juu ya taarifa za kugunduliwa kwa makaburi waliyozikwa watu wengi kwa pamoja.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman