1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuelekea barani Afrika kutafuta mafuta

Josephat Charo 11 Januari 2008

Huku Marekani ikiwa inatumia kiwango kikubwa cha mafuta duniani, bado inataka kuwa na mafuta zaidi.

https://p.dw.com/p/CoS8
Kiwanda cha mafuta cha Heglig karibu na Bentiu, kusini mwa SudanPicha: AP

Bei ya mafuta imefikia dola 100 kwa pipa. Dhahabu hiyo nyeusi imekuwa na bei ya juu mno ambayo haijawahi kutokea. Wawindaji wa mafuta wameanza kulikodolea macho bara la Afrika, zikiwemo Marekani na China ambazo zinataka kuwa na uhakika wa mahitaji yao ya mafuta barani humo.

Marekani inatumia kiwango kikubwa cha mafuta duniani na inataka kuwa na mafuta zaidi. India na China zinataka pia kuwa na mafuta mengi zaidi kwa idadi kubwa ya wananchi wao. Kati ya China na Marekani kumezuka mashindano ya kupigania nishati ya mafuta katika kila pembe ya dunia.

Katika miaka michache iliyopita, Afrika haikuwa na umuhimu mkubwa katika sera za nje za Marekani. Lakini sasa inataka kuanza kuwekeza katika bara hilo.

Nancy Walker, mtaalamu wa maswala ya siasa na aliyekuwa zamani kiongozi wa afisi iliyoshughulikia maswala ya Afrika katika wizara ya ulinzi ya Marekani anasema mafuta ndiyo sababu kubwa ya Marekani kutaka kuwa na maslahi yake barani Afrika.

´Mafuta ni mojawapo ya sababu kwa nini Marekani ina masilahi yake barani Afrika. Ukiangalia mkakati wa usalama wa Marekani utaona unazungumzia usalama wa nishati. Mahali popote palipo na raslimali za mafuta, panakuwa muhimu kwa maslahi ya Marekani.´

Kwa mujibu wa mkakati wa usalama wa Marekani wa mwaka wa 2002, Afrika itakuwa kituo muhimu kitakachohakikisha mahitaji ya nishati ya Marekani yanatoshelezwa. Hapo kabla eneo la Afrika magharibi lilikuwa eneo lililokua kwa kasi katika usafirishaji wa mafuta na gesi nchini Marekani.

Mbali na Nigeria, nchini Sao Tome na Principe katika ghuba ya Guinea kuligunduliwa mafuta katika miaka ya nyuma na huko nchini Mali na Mauritania, kukagunduliwa gesi. Juu ya hayo, wataalamu wanadhani kuna mafuta na gesi katika eneo la Sahara Magharibi.

Miaka sita iliyopita Marekani ilianzisha kambi ya jeshi lake barani Afrika huko nchini Djibouti. Kutoka nchini humo Wamarekani hulidhibiti eneo la bahari linalotumiwa kwa usafiri wa meli. Asilimia 25 ya mafuta yote duniani husafirishwa kupitia eneo hilo. Zaidi ya hayo, Djibouti iko karibu na bomba kubwa la mafuta la Sudan.

Werner Ruf, mtaalamu wa maswala ya Afrika na profesa wa uhusiano wa kimataifa na sera za kigeni katika chuo kikuu cha Kassel hapa Ujerumani, anaeleza umuhimu wa mafuta ya Afrika mwa Wamarekani.

Kilele cha akiba ya mafuta duniani kimefikiwa au kimepitwa na mashindano ya kuwania mafuta yatazidi. Marekani inapanga asilimia 13 ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje yatoke Afrika kufikia mwaka wa 2013, hivyo katika miaka 6 hadi 7 kiwango hicho kitapanda na kufikia asilimia 25. Afrika itakuwa msafirishaji mkubwa wa mafuta kwa Marekani.´

Makadirio yanaonyesha pato jumla la mafuta barani Afrika ni mapipa bilioni moja zaidi ikilinganishwa na kiwango nchini Irak. Tathmini hiyo inaifanya Afrika kuvutia zaidi. Ndio maana China imekuwa katika miaka iliyopita ikipanua uhusiano wake na nchi za kiafrika.

Marekani inajaribu tangu kikwazo cha mafuta kilichowekwa na Waarabu mnamo mwaka wa 1973 kutafuta wasafirishaji mbalimbali wa mafuta. Kijiografia Afrika ina jukumu muhimu kwani njia ya mojamoja kutoka barani humo kwenda Marekani inaongeza uhakika wa kutosheleza mahitaji ya Wamarekani.

Kwa muda wa mwaka mmoja uliopita wizara ya ulinzi ya Marekani imekuwa na jeshi lake barani Afrika, Africom. Makao makuu ya jeshi hilo ni mjini Stuttgart hapa Ujerumani. Bado Wamarekani wanatafuta makao makuu ya jeshi hilo barani Afrika.

Lengo rasmi la jeshi hilo ni kusaidia ushirikiano wa pamoja kati ya Marekani na nchi za kiafrika katika maswala ya usalama. Mtaalamu wa maswala ya Afrika Werner Ruf anaonya.

´Marekani inaamini pengine kupitia msaada wa kuwepo majeshi yake itakuwa na uhakika wa kupata nishati. Lakini kwa maoni yangu kuna uwezekano mdogo wa hilo kutokea. Kuwepo kwa majeshi ya Marekani katika maeneo haya kunaweza kusababisha upinzani na kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi ambacho kimo katika mpango wa jeshi la Marekani barani Afrika, Africom, kinaweza kusababisha matokeo yasiyotarajiwa. Magaidi wanaweza kujitokeza iwapo Marekani itakuwa na idadi kubwa ya wanajeshi.´

Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf amependekeza kwa Marekani kwamba nchi yake ingependa kuwa makao makuu ya jeshi la Africom, lakini nchi nyingine hazijasema lolote kuhusu jeshi hilo.

Katika msimu wa kiangazi uliopita Algeria, Moroko na Libya zilipinga jeshi hilo la Africon barani Afrika.

Nchi 14 wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, zimekataa kambi ya jeshi la Africom kujengwea katika ardhi zao.