1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuirejesha Syria katika baraza la usalama...

9 Septemba 2013

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, amesema nchi yake haiondowi uwezekano wa kurudi katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupata suluhisho juu ya Syria, baada ya kukamilika kwa ripoti ya wakaguzi

https://p.dw.com/p/19dym
John Kerry na Laurent Fabius.
John Kerry na Laurent Fabius.Picha: LIONEL BONAVENTURE/AFP/Getty Images

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Paris Ufaransa, Kerry alisema rais Barack Obama bado hajafanya uamuzi kuhusu suala hilo. Tawala mjini Washington na Paris zinasema vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad vilihusika na shambulizi la Agosti 21, ambamo zaidi ya watu 1,400 waliuawa, na zinatafakari kufanya mashambulizi ya angani ili kujaribu kumzuia Assad kutotumia silaha hizo tena.

Marais Vladmir Putin na Barack Obama wakati wa Mkutano wa kilele wa G20 mjini Moscow.
Marais Vladmir Putin na Barack Obama wakati wa Mkutano wa kilele wa G20 mjini Moscow.Picha: picture-alliance/dpa

Kerry aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kuwa Saudi Arabia, ambayo imekuwa mmoja wa wapinzani wakubwa wa rais Assad, na ambayo wanadiplomasia wanasema ni mmoja wa wagavi wakuu wa silaha kwa waasi wa Syria, imeunga mkono mashambulizi ya kijeshi, na kwamba wanaunga mkono kuchukuliwa kwa hatua.

"Kama tulivyojadiliana leo, sote tumekubaliana, na hakuna hata mmoja aliepinga, kuwa matumizi ya silaha za kemikali na utawala wa Assad, ambayo tunajua yaliwauwa mamia ya watu wasio na hatia, wakiwemo watoto wasiopungua 426 katika tukio hilo, hili linavuka msitari mwekundu wa kimataifa. Na tunakubaliana kuwa kukiuka taratibu za kitaasisi ambazo jamii ya kimataifa imeziheshimu kwa karibu karne nzima, ni muhimu kuwa hizo zinasimamiwa," alisema waziri Kerry.

Rais wa Ufaransa, ambaye anazidi kukabiliwa na shinikizo nyumbani na miongoni mwa washirika wake wa Ulaya kutafuta idhini ya Umoja wa Mataifa kabla ya kuingilia kijeshi nchini Syria, alisema siku ya Jumamosi kuwa angetafuta azimio la baraza la usalama licha ya Urusi na China kuyapigia kura za turufu, maazimio yaliyopita.

Mawaziri John Kerry (kulia) na Chuck Hagel wakitoa maelezo kwa kamati ya Bunge la Marekani kutetea hatua za kijeshi dhidi ya Syria.
Mawaziri John Kerry (kulia) na Chuck Hagel wakitoa maelezo kwa kamati ya Bunge la Marekani kutetea hatua za kijeshi dhidi ya Syria.Picha: Getty Images

China yataka tahadhari ichukuliwe
Waziri wa mambo ya kigeni wa China, Wang Yi alimuambia Waziri Kerry katika mazungumzo kwa njia ya simu usiku wa Jumapili, kuwa ipo haja ya kuchukua tahadhari katika kushughulikia suala la Syria, akishauri suala hilo lirudishwa katika baraza la usalama.

Matamshi ya Wang Yi yanakuja baada ya rais wa China Xi Jinping kumuambia rais Barack Obama wakati wa mkutano wa mataifa yanayounda kundi la G20 nchini Urusi Ijumaa wiki iliyopita, kuwa mashambulizi ya kijeshi hayatatatua mgogoro wa Syria, na kwamba suluhu ya kisiasa ndiyo njia sahihi ya kuondoka katika mkwamo huo.

Ripoti ya uchunguzi wiki hii
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wanatarajiwa kukabidhi ripoti yao mwishoni mwa wiki hii, wakati bunge la Marekani likijadili uwezekano wa kuruhusu mashambulizi yenye mipaka dhidi ya Syria. China imekuwa ikisisitiza haja ya kufanyika kwa uchunguzi huru katika shambulizi hilo, na imeonya dhidi ya kuhukumu kabla ya kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi huo. Ilisema pia kuwa yoyote alietumia silaha hizo laazima awajibishwe.

Shirika la habari la serikali ya China lilisema siku ya Jumatatu kuwa kampeni ya kushawishi matumizi ya nguvu haina mashiko, na kwamba shambulio dhidi ya Syria litakuwa ukiukwaji wa sheria ya kimataifa. "Wakati umefika sasa wa kuacha busara itumike kuliko uzembe," lilisema shirika la habari la Xinhua, katika tahriri, inayoakisi mawazo rasmi ya serikali ya China.

Mbali na kura yake ya turufu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, China imekuwa makini kuonyesha kuwa haiegemei upande katika mgogoro wa Syria, na imekuwa ikiisihi serikali kuzungumza na wapinzani, na pia kuchukua hatua kutekeleza matakwa ya kufanya mageuzi ya kisiasa. Imesema pia kuwa ipo haja ya kuunda serikali ya mpito.

Muonekano wa manowari ya kubeba ndege za kivita ya Nimitz, ambayo imehamishiwa katika bahari nyekundu katika maandalizi ya mashambulizi dhidi ya Syria.
Muonekano wa manowari ya kubeba ndege za kivita ya Nimitz, ambayo imehamishiwa katika bahari nyekundu katika maandalizi ya mashambulizi dhidi ya Syria.Picha: Reuters

Assad amshukuru Putin
Wakati huo huo, rais Bashar al-Assad ametoa shukrani kwa rais wa Urusi Vladmir Putin kwa kusimama upande wake wakati wa mazungumzo ya mataifa ya G20 wiki iliyopita, waziri wa mambo ya kigeni wa Syria amesema mjini Moscow.

"Rais amenituma nifikishe shukrani zake kwa Putin kwa msimamo wake wakati na baada ya mkutano wa G20," alisema waziri Walid el Muallem wakati wa kuanza kwa mazungumzo kati yake na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow.

Kerry aendeleza juhudi za kidiplomasia
Waziri Kerry yuko nchini Uingereza leo, kuendeleza juhudi za Marekani kutafuta uungwaji mkono wa hatua za kijeshi nchini Syria, na alitarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya kigeni William Hague, na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas mjini London. Bunge la Uingereza lilipiga kura dhidi ya kuingilia kijeshi nchini Syria wiki iliyopita.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae, rtre,ape
Mhariri: Charo Josephat Nyiro