1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiondoa huko kulianza tangu Trump aingie madarakani

Admin.WagnerD4 Desemba 2017

Mara baada ya Rais Donald Trump kushika usukani wa kuiongoza Marekani, taifa hilo lenye nguvu limeonekana kujitoa katika ajenda mbalimbali ikiwamo mikataba ya kimataifa .Hali iliyozua wasiwasi wa nafasi yake kidunia.

https://p.dw.com/p/2okJQ
USA Präsident Donald Trump
Rais wa Marekani, Donald Trump.Picha: Reuters/J. L. Duggan

Ni Marekani kwanza au Marekani peke yake. Hicho ndicho kinachohojiwa mara baada ya Rais Trump kuingia madarakani Januari mwaka huu. Tangu Trump aingie madarakani, Marekani imejiondoa au kutishia kujiondoa katika mikataba mbalimbali ya kimataifa,  ikisimamia sera yake ya Marekani kwanza.

Washauri wa Trump wamesisitiza kuwa kauli mbiu ya ´Marekani Kwanza´ haiashirii   msimamo wowote wa kujitenga,  hata hivyo kumeibuka tabia za kutojihusisha na  kutowajibika katika nyanja mbalimbali za kimataifa.

Jumamosi iliyopita, serikali ya Trump ilitangaza kujitoa katika makubaliano ya Umoja wa Mataifa ya kuimarisha  usimamizi wa wakimbizi na wahamiaji. Hatua iliyoonekana kuwa ni kutokuwa na msimamo katika sera zake.

 Richard Haass,  aliyekuwa Mkurugenzi wa Sera na mipango katika Wizara ya Mambo ya nje , wakati wa utawala wa Rais George W. Bush, ameuita utawala wa Trump kuwa ni.  ´mafundisho ya kujitenga´.

 Baadhi ya makubaliano ambayo Trump amejiondoa au kutishia kujiondoa ni pamoja na uamuzi wa Jumamosi wiki iliyopita ambapo  ujumbe wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, ulitangaza kuwa Marekani inasitisha ushiriki wake mpango wa dunia kuhusu uhamiaji.

Septemba mwaka jana, wanachama 193 wa baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa shauri moja walikubaliana kuhusu  maazimio ya kisiasa yasiyofungamana na upande wowote.

Mengine ni azimio la New York kwa wakimbizi na wahamiaji, wakiahidi  kutekeleza  haki za wakimbizi, kuwasaidia kupata makazi na kuhakikisha wanapata elimu na ajira.

Makubaliano hayo ya jumla, yaliyojikita katika azimio hilo, yanatarajiwa kuwasilishwa katika Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  mwakani.

Lakini  ujumbe wa Marekani umesema azimio hilo,  limejawa mipango kadhaa isiyoendana na sera za uhamiaji na wakimbizi za Marekani na sheria za uhamiaji za utawala wa Trump.

USA UN Generalversammlung in New York Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, katika kipindi cha mjadala wakati wa kikao cha 70 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.Picha: picture-alliance/newscom/J. Angelillo

 Kujiondoa kwa Marekani kutoka shirika la Unesco

Pamoja na hilo, Oktoba mwaka huu, serikali hiyo ya Marekani ilisema itajiondoa katika shirika la Umoja wa Mataifa la kusimamia elimu,Sayansi na utamadun Unesco ikilishutumu kwa kuionea Israel.

Kujiondoa huko kutaanza rasmi mwishoni mwa mwaka ujao, wakati ambapo Marekani, itaanzisha ´mjumbe mwangalizi´  atakayekuwa mbadala wa mwakilishi wa  UNESCO.

Kadhalika, mwezi Juni Trump alitangaza kuwa Marekani itajiondoa katika  makubaliano ya Paris yaliyohusisha nchi 196 kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na akataka majadiliano ya mpango mpya wa kiulimwengu.

 Alilamika kuwa makubaliano hayo yanazipa nchi nyingine umuhimu usio  wa haki katika suala la viwanda vya Marekani na hivyo kuharibu kazi za Wamarekani.  Lakini hata kujiondoa huku nako kutaanza kutekelezwa, Novemba 2020.

Ukiachilia mbali hilo, siku chache tu baada ya kuingia madarakani, Trump aliiondoa Marekani katika  makubaliano ya biashara huru ya nchi za Pasifiki, TPP).

Ulikuwa ni muswada mkubwa wa kibiashara duniani, na ulisainiwa Februari 2016 kwa kushirikiana na  nchi 11 za Asia na Pasifiki, isipokuwa China.

 Kielelezo kingine kinachoonyesha kuwa Marekani, inataka kuwa peke yake, ni kuondoa ushiriki wake katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia, yaliyotiwa saini, Julai 2015 na Iran pamoja na nchi zenye nguvu duniani. Nchi hizo zikiwa ni  pamoja na Uingereza , China, Ufaransa; Urusi, Marekani yenyewe na Ujerumani.

 Hatima ya mkataba huo kwa sasa ipo mikononi mwa  bunge la Marekani, ambalo litaamua kuuvunja au  kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Kadhalika Trump ameamuru majadiliano mapya kuhusu makubaliano ya Biashara Huria ya Kaskazini mwa Marekani,(NAFTA) ya mwaka 1994,  pamoja na Mexico na Canada, ambayo ameyaita kuwa ni mkataba mbaya uliowahi kusainiwa.

Mazungumzo yalianza Agosti, lakini Trump, alitishia kujiondoa katika makubaliano hayo na kujadili masuala ya ubia.

 Pamoja na mambo mengine, Rais huyo wa Marekani anataka mabadiliko katika kile anachokiita ´urasimu´ unaofanywa na Umoja wa Mataifa, huku akilishutumu shirika hilo kwa usimamizi mbaya.

Mwandishi: Florence Majani(AFP)

Mhariri: Saumu Yusuf