1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na China zakubaliana kushirikiana zaidi

12 Novemba 2014

Rais wa China Xi Jinping amesema amefanya mazungumzo yenye tija na Rais wa Marekani Barack Obama na nchi hizo mbili zimekubaliana kuharakisha mazungumzo kuhusu uwekezaji wa pamoja na kuboresha uhusiano wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/1DlfN
Picha: Reuters

Rais Xi amesema China na Marekani zimekubaliana kuchukua hatua za kuimarisha uhusiano katika masuala muhimu yatakayojenga imani kati yao kama ulinzi na ushirikiano katika kupambana na ugaidi.

Nchi hizo mbili pia zimekubaliana kuhusu ushirikiano wa kuimarishwa kwa sheria ikiwemo kukabiliana na uhalifu wa kuvunjwa kwa sheria za kimataifa.

Marekani yasema iko tayari kushirikiana na China

Rais wa Marekani Barack Obama amesema licha ya Marekani na China kuwa washindani, miamba hao wawili wa kiuchumi duniani wanaweza kufanya kazi kwa pamoja katika masuala watakayokubaliana ili kuimarisha usalama wa raia wao.

Rais wa Marekani Barack Obama na Rais wa China Xi Jinping
Rais wa Marekani Barack Obama na Rais wa China Xi JinpingPicha: Reuters/G. Baker

Xi na Obama wameyasema hayo hii leo katika mkutano na wanahabari mjini Beijing, China baada ya mazungumzo ya siku mbili kuhusu masuala ya kiuchumi na usalama kati yao.

Obama ametangaza katika mkutano huo kuwa nchi yake itapunguza kiwango cha gesi chafu inayotoka viwandani na China kwa upande wake imeahidi itachukua hatua madhubuti kupunguza gesi hiyo inayoharibu mazingira kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa, hatua ambayo imetajwa kuwa ya kihistoria kufuatia kujivuta kwa China kujitolea kufanya hivyo katika kipindi cha nyuma.

Obama amesema hatua hiyo ni ufanisi mkubwa katika uhusiano wa nchi hizo mbili na inaonyesha kile kinachoweza kufikiwa iwapo zitashirikiana kushughulikia changamoto kubwa zinazoukumba ulimwengu.

Tangazo hilo la kupunguza gesi chafu kutoka viwandani kutoka China na Marekani ambazo ni miongoni mwa wachafuzi wakubwa duniani wa mazingira zinaonyesha kujitolea kwa nchi hizo mbili katika kushughulikia tatizo hilo ambalo limepandisha viwango vya joto duniani lakini jinsi zitavyofikia shabaha hiyo bado inasubiriwa kuonekana itakuwa vipi.

Nchi zote mbili kupunguza uchafuzi wa mazingira

Marekani imeweka malengo ya kupunguza gesi hiyo kwa kati ya asilimia 26 hadi 28 ifikapo mwaka 2025 ikilinganishwa na viwango ilivyoviweka mwaka 2005 vya kuipunguza kwa asilimia 17 ifikapo mwaka 2020.

Gesi chafu ikitoka viwandani China
Gesi chafu ikitoka viwandani ChinaPicha: picture-alliance/dpa

Aliyekuwa makamu wa Rais wa Marekani Al Gore amelitaja tangazo hilo kama hatua kubwa katika kuelekea kuutatua mzozo wa madhara ya mabadiliko ya hewa ulimwenguni.

Hata hivyo wanasiasa wa chama cha Republican nchini Marekani wamesema watapinga mpango huo kwa hoja kwamba Obama ataawachia marais wa siku za usoni nchini humo mzigo wa kulifikia lengo hilo ambalo ni gumu mno.

Obama amegusia pia kuhusu umuhimu wa watu wa Hong Kong kushiriki katika uchaguzi huru na wa haki huku Xi akisema hilo ni suala la ndani la China kulishughulikia.

Viongozi hao wanatarajiwa baadaye leo kuhudhuria mkutano wa kibiashara wa nchi za kusini mashariki mwa bara Asia unaofanyika leo nchini Myanmar.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Ap

Mhariri: Gakuba Daniel