1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na China zakwaruzana

12 Desemba 2016

China imeelezea kutoridhishwa kwake na mapendekezo ya rais mteule Donald Trump kwamba atafutilia mbali sera ya Marekani kuhusu China moja iwapo serikali ya Beijing haitaridhia masuala mbali mbali yakiwemo ya kibiashara.

https://p.dw.com/p/2U7s0
Kombobild Trump und Tsai Ing-wen
Picha: Getty Images/T. Wright/A. Pon

Msemaji wa wizara ya masuala ya nchi za kigeni wa China Geng Shuang amesema kuwa iwapo sera hiyo ya China Moja inayotoa muongozo wa uhusiano kati ya serikali ya Beijing na eneo lenyE mamlaka yake ya ndani la Taiwan itabatilishwa ama kutatizwa, uhusiano kati ya China na Marekani pamoja na ushirikiano wa sekta mbali mbali kati ya mataifa hayo mawili utakuwa jambo gumu kutekeleza.
Serikali ya China inalichukulia eneo la Taiwan kuwa muhimu sana katika uhuru wake na ulinzi wa mipaka yake na kuongeza kuwa uzingatiaji wa sera hiyo ya China Moja ndicho kigezo cha kisiasa katika uhusiano wake na Marekani.
Shuang aliongeza kuwa matamshi hayo ya Trump wakati wa mahojiano kupitia  runinga mwishoni mwa juma, yanatishia kusambaratisha uhusiano kati ya Marekani na China.

China Donald Trump auf Titelseite einer Zeitschrift
Kichwa cha gazeti moja nchini China. Trump ataibadilisha vipi dunia?Picha: Getty Images/AFP/G. Baker


Lakini kulingana na Trump, haoni sababu ya kuzingatia sera hiyo ya China moja iwapo hawatakubaliana na China kuhusiana na masuala mbali mbali ikiwemo biashara. Aliilaumu China kwa kuiumiza Marekani na pia kutetea vikali hatua ya kuwasiliana kwa njia ya simu na Tsai Ing-Wen, rais wa eneo lenye mamlaka yake ya ndani kidemokrasia la Taiwan mapema mwezi huu, eneo ambalo halijadhibtiwa na Beijing kwa zaidi ya miaka 60.
Ijapokuwa Marekani ni mshirika mkuu wa Taiwan na msambazaji wake wa silaha, Marekani haijakuwa na uhusiano  rasmi wa kidiplomasia na eneo hilo tangu mwaka 1976 ilipoanza kuitambua Beijing.

 
Mwandishi: Tatu Karema
Mhariri:Yusuf Saumu