1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi "Vinara" biashara ya silaha

Admin.WagnerD20 Februari 2017

Marekani na Urusi zinatajwa kuwa vinara wa kuuza silaha kwa zaidi ya nusu ya biashara yote duniani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambacho kimeshuhudia biashara ya silaha ikifikia kiwango cha juu zaidi

https://p.dw.com/p/2XtMh
Symbolbild SIPRI Militärausgaben Bericht 2014
Picha: picture-alliance/dpa

Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya kimataifa ya masuala ya amani, inayofuatilia biashara ya silaha duniani, SIPRI inaonyesha kuongezeka kwa biashara  ya silaha na kufikia kiwango cha juu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tangu kumalizika kwa vita baridi. Ongezeko hilo limechangiwa zaidi na kupanda kwa mahitaji yatokanayo na mzozo wa Mashariki ya Kati na Asia.

Kulingana na taasisi hiyo yenye makao yake mjini Stockholm, Sweden, katika kipindi cha mwaka 2012 na 2016, uagizaji wa silaha kwa kuzingatia wingi katika nchi za Asia na zilizozungukwa na Bahari ya Pacific, zinazojulikana kama  nchi za Oceania ilifikia asilimia 43 ya biashara ya silaha duniani. Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 7.7 ikilinganishwa na kipindi cha kati ya mwaka 2007-2011.

"Uuzaji wa silaha kubwa katika kipindi cha mwaka 2012-16 ulifikia kiwango cha juu kabisa ambacho hakijashuhudiwa katika kipindi chochote cha miaka mitano tangu kumalizika kwa vita baridi", taasisi hiyo binafsi imesema.

Mgawo wa uingizwaji wa silaha hizo kimataifa katika mataifa ya Asia na Oceania ulipanda kiasi kati ya mwaka 2007 na 2011, huku mgawo katika nchi za Mashariki ya Kati na Falme za Ghuba ukipanda kutoka asilimia 17 hadi 29, mbele zaidi ya Ulaya, kwa asilimia 11, Amerika kwa asilimia 8.6 na Afrika kwa asilimia 8.1.

Infografik Weltweit größte Waffenexporteure Englisch

"Katika kipindi cha miaka mitano, mataifa mengi yaliyopo ukanda wa Mashariki ya Kati kimsingi yameyageukia mataifa ya Marekani na Ulaya katika harakati zao za kujiwezesha kijeshi" amesema Mtafiti mwandamizi wa programu ya silaha na matumizi yake ndani ya SIPRI, Pieter Wezeman.

Pamoja na kushuka kwa bei za mafuta, mataifa katika ukanda huo yameendelea kuagiza silaha nyingi zaidi katika mwaka wa 2016, na kuzitumia kama zana muhimu katika kukabiliana na mizozo na hali ya wasiwasi wa kikanda, ameongeza.

SIPRI imesema, biashara ya silaha kimataifa ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita imefikia rekodi ya juu zaidi tangu mwaka 1950. Saudi Arabia, ilikuwa ni ya pili katika biashara ya uingizwaji wa silaha, ikiwa nyuma ya India, tofauti na China ambayo bado haitengenezi silaha kwa kiwango cha kitaifa.

Marekani inasalia kuwa nchi inayoongoza kwa uuzaji wa silaha kwa asilimia 33, mbele ya Urusi yenye asilimia 23, China ina asilimia 6.2 na Ufaransa ikiwa na asilimia 6.0 huku Ujerumani ikifikia asilimia 5.6. Mataifa haya matano yanafanya asilimia 75 ya mauzo ya nje ya silaha nzito duniani.

Kupanda kwa kiwango cha mauzo ya nje ya Ufaransa kunafuatia makubaliano ya mkataba na Misri iliyoagiza meli na ndege za kivita. Mkuu wa programu ya zana za silaha katika taasisi hiyo Aude Fleurant ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kuna ushindani mkali miongoni mwa nchi zinazozalisha silaha Barani Ulaya, wakati ambapo Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zikiongoza.

Marekani na Ufaransa zimesalia kuwa wasambazaji wakubwa katika Ukanda wa Mashariki ya Kati, wakati Urusi na China wakifanya mauzo makubwa ya nje katika nchi za Asia. Urusi iliuza silaha kwa mataifa 50, ingawa theluthi mbili ya mauzo yake ya nje yalikwenda India, Vietnam, China na Algeria.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman