1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini kuchukuliwa hatua madhubuti

7 Januari 2016

Marekani na washirika wake wakuu wawili wa kijeshi barani Asia - Korea Kusini na Japan, wametishia kuchukua hatua madhubuti dhidi ya kitendo cha Korea Kaskazini cha kufanya jaribio lililofanikiwa la bomu la nyuklia.

https://p.dw.com/p/1HZcr
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong UnPicha: picture-alliance/dpa

Viongozi wa nchi hizo tatu, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta namna ya kuungana kupinga vitisho vya nyuklia vinavyotolewa na Korea Kaskazini, walizungumza kwa njia ya simu siku moja baada ya nchi hiyo kutangaza kwamba imefanya jaribio la kwanza la bomu la nyuklia, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali kimataifa.

Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini, Han Min Koo amezungumza na mwenzake wa Marekani, Ash Carter, ambapo wote wawili walikubaliana kuchukua hatua madhubuti dhidi ya kitendo cha uchokozi cha Korea Kaskazini. Hata hivyo haijafahamika mara moja hatua zitakazochukuliwa. Koo amesema mazoezi ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili bado yataendelea.

''Tumekubaliana kuendelea na mazoezi ya kijeshi yaliyopangwa na kuanzisha mkakati wa kuzuia makosa yasitendeke kwa Korea Kusini na Marekani, pamoja na mfumo wa hatua za kijeshi wa kuchunguza, kuvuruga na kujilinda,'' alisema Koo.

Rais wa Marekani, Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Martinez Monsivais

Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani, Rais Barack Obama leo amezungumza na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, kuhusu kuchukuliwa hatua za kimataifa kutokana na kitendo hicho cha Korea Kaskazini.

Obama na dhamira yake kwa usalama wa washirika wake

Rais Obama amemhakikishia dhamira ya Marekani kuhusu usalama wa Japan na viongozi hao wawili wamekubaliana kufanya kazi kwa pamoja kuchukua hatua kali za kimataifa kujibu kitendo cha uchokozi cha Korea Kaskazini.

Aidha, Rais Obama amezungumza pia na Rais wa Korea Kusini, Park Geun-Hye, ambaye amelaani vikali kitendo cha Korea Kaskazini alichokiita kuwa ni cha uchochezi. Park ametaka hatua kali za kimataifa zichukuliwe dhidi ya nchi hiyo.

Mazungumzo kati ya viongozi wa Marekani, Korea Kusini na Japan, yamefanyika baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 kukutana mjini New York na kulaani vikali jaribio hilo la Korea Kaskazini. Baraza hilo limesema litaanza kuifanyia kazi rasimu ya azimio jipya la Umoja wa Mataifa litakalohusisha hatua kali zaidi za kuiadhibu nchi hiyo kutokana na kitendo chake cha uchokozi.

Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha kwamba mazungumzo yanaendelea kujadiliana namna ya kuimarisha zaidi vikwazo kadhaa ambavyo viliwekwa dhidi ya Korea Kaskazini tangu nchi hiyo ilipofanya jaribio la kwanza la bomu la atomiki mwaka 2006. Baraza hilo limesema jaribio la hivi karibuni la Korea Kaskazini ni tishio kwa usalama na amani ya kimataifa na nchi hiyo imekuwa ikikaidi maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Franklin II

Hata hivyo wataalamu wa masuala ya silaha za nyukilia wamesema bomu hilo la nyuklia halikuwa na nguvu kubwa namna hiyo kama ambavyo Korea Kaskazini imedai. Wamesema bomu hilo lilikuwa dogo linalokadiriwa kuwa na nguvu kati ya sita hadi tisa katika kipimo cha kiloton. Utafiti wa awali ambao umefanywa unaonyesha kutofautiana na madai ya Korea Kaskazini kwamba imefanikiwa katika jaribio hilo na hakuna kitu kama hicho kilichotokea katika muda wa saa 24.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef