1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani tayari kwa suluhisho la kijeshi dhidi ya IS

23 Januari 2016

Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden Jumamosi (23.01.2016) amesema kwamba Marekani na Uturuki ziko tayari kwa suluhisho la kijeshi dhidi ya Dola la Kiislamu iwapo usuluhishi wa kisiasa utashindwa kupatikana Syria.

https://p.dw.com/p/1Hiwc
Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden(kushoto) na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Istanbul. (23.01.2016)
Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden(kushoto) na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu mjini Istanbul. (23.01.2016)Picha: picture-alliance/dpa/S. Suna

.Kauli hiyo inakuja wakati duru mpya ya mazungumzo ya kutafuta amani nchini Syria ikiwa mashakani. Mazungumzo hayo yamepangwa kuanza Jumatatu mjini Geneva lakini yako hatarini kuahirishwa kutokana na nani watakaounda ujumbe wa upinzani.

Biden akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema " Tunajuwa ingelikuwa vyema iwapo tutaweza kufikia suluhisho la kisiasa lakini tumejiandaa .... iwapo hilo halitowezekana kuwa na suluhisho la kijeshi katika operesheni hii ya kulin'gowa kundi la Daesh."

Kwa kiarabu waasi wa kundi la Dola la Kiislamu wanatambulika kwa jina hilo la Daesh ambalo linashikilia maeneo makubwa ya Syria.Afisa wa Marekani baadae amefafanuwa kwamba Biden alikuwa akimaanisha suluhisho hilo la kijeshi kwa kundi la Dola la Kiislam na sio Syria kwa jumla.

Kuimarisha upinzani

Upinzani unaoungwa mkono na Saudi Arabia umefuta uwezekano wa kuwa na mazungumzo ambayo hata yasio ya moja kwa moja venginevyo serikali ya Syria inachukuwa hatua ikiwa ni pamoja na kusitisha mashambulizi ya anga yanayofanywa na Urusi.

Muungano wa wapiganaji waasi nchini Syria.
Muungano wa wapiganaji waasi nchini Syria.Picha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Biden amesema yeye na Davutoglu pia wamejadili vipi washirika hao wawili katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanavyoweza kusadia zaidi makundi ya waasi wa madhehebu ya Sunni yanayopambana kumpinduwa Rais Bashar al Assad.

Saleh Muslim mwenyekiti mwenza wa Chama cha Demokrasia cha Wakurdi (PYD) ambacho ni chama kikuu cha kisiasa cha Wakurdi nchini Syria amesema hapo Ijumaa kwamba mazungumzo ya amani ya Syria yatashindwa iwapo Wakurdi hao wa Syria hawatowakilishwa.

Kutofautiana juu ya kundi la Wakurdi

Wakati Marekani inatafautisha kati ya kundi hilo la PYD ambapo wapiganaji wake inawaunga mkono na chama kilichopigwa marufuku cha Wafanyakazi wa Kikurdi PKK kilioko nchini Uturuki ,Davutoglu amesisitiza msimamo wa Uturuki kwamba tawi la kijeshi la chama cha PYD ni sehemu na linaungwa mkono na chama cha PKK cha Wakurdi wa Uturuki.

Tawi la kijeshi la chama cha PYD yaani Vikosi vya Ulinzi wa Wananchi kama vinavyojulikana (YPG) vimenyakuwa maeneo makubwa ya Syria kutoka kundi la Dola la Kiislamu kwa msaada wa mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Marekani na kuyatangaza kuwa yako chini ya mamlaka yake.Davutoglu amesema YPG imezidi kuwa tishio kwa Uturuki.

Wapiganaji wa Kikurdi wa kundi la YPG.nchini Syria.
Wapiganaji wa Kikurdi wa kundi la YPG.nchini Syria.Picha: picture alliance/dpa/S. Suna

Serikali ya Uturuki imekuwa katika mapambano ya miongo mingi ya uasi dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi wanaotaka kujitenga wa chama cha PKK ambapo hapo mwezi wa Julai kulikuwa na makabiliano mapya yaliosababisha maafa na vikosi vya usalama vya Uturuki.

Biden amekishutumu vikali chama cha PKK ambacho kimeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, Umoja wa Ulaya na Uturuki.

"ISIL (Dola la Kiislamu) sio tu tishio pekee la kuwepo kwa uhai PKK pia ni tishio kama hilo na tunalitambuwa hilo."

amesema Biden na kuongeza" PKK haikuonyesha shauku wala ishara ya kutaka kuishi kwa amani.Ni kundi la kigaidi tu na kile wanachoendelea kutenda kinakirihisha kabisa."

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Daniel Gakuba