1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Urusi na Ujeurmani zakubali kuhusu Iran

Maja Dreyer22 Februari 2007

Suala la mradi wa kinyuklia wa Iran lilizungumziwa kwenye mkutano baina ya mawaziri wa nchi za nje wa Ujerumani, Marekani na Urusi uliofanyika leo hii mjini Berlin. Wakati huo huo shirika la kudhibiti nishati ya nyuklia linatarajiwa kutoa ripoti yake mpya juu ya mradi huo huo.

https://p.dw.com/p/CHJS
Sergej Lawrow na Frank-Walter Steinmeier
Sergej Lawrow na Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Baada ya mkutano wa pande nne zinazojishughulikia na mzozo wa Mashariki ya Kati uliofanyika mjini Berlin jana, wanasiasa wa vyeo vya juu bado wako Berlin kuendelea na mazungumzo ya ana kwa ana. Leo hii waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, alikutana mwenzake wa Urusi, Sergej Lawrow. Wote wawili wasisitiza umuhimu kwa nchi hizo mbili kuafikiana juu ya masuala mazito ya siasa za kimataifa.

Ni Frank-Walter Steinmeier: “Katika siku kama hizo tukiwa na mazungumzo ya pande nne kuhusu Mashariki ya Kati, tukiwa na mizozo ya Iran na Mashariki ya Kati, tunaona vile tunavyotegemeana. Mizozo hiyo inatuonyesha kwama Ulaya na Urusi zinahitajikana.”

Ujeruman na Urusi, na vile vile waziri wa nchi za nje wa Marekani, Condoleezza Rice pamoja na mwakilishi wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, wote walisema kuwa wako tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo kuhusiana na mradi wa kinyuklia wa Iran ikiwa masharti fulani yatatimizwa. Waziri Steinmeier alisema kuna matumaini kuwa Iran itafahamu kuwa hata mradi mkubwa wa kinyuklia hauwezi kuwalisha watu wake. Wanasiasa hawa waliokutana mjini Berlin walikubaliana kuendelea na mazungumzo ya karibu na kuafikiana juu ya hatua zitakachochukuliwa katika siku zijazo.

Shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya kinyulia, IAEA, linataka kutoa ripoti yake mpya juu ya mradi wa kinyuklia wa Iran baadaye leo hii. Katika ripoti yake, shirika la IAEA linatarajiwa kuweka wazi kuwa Iran ilipanua mradi wake wa kinyuklia badala ya kuusitisha. Ripoti hii ambayo tayari jana ilitarajiwa kuchapishwa itakuwa msingi kwa uamuzi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea Iran vikwazo. Mawaziri wa Ujerumani, Urusi na Marekani lakini pia wamesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa itajaribu kuishawishi Iran kukubali mazungumzo mapya.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alielezea wasiwasi kubwa kuhusu msimamo wa Iran katika mzozo huu. Ban ambaye leo mchana alikutana na Kansela Merkel wa Ujerumani na baadaye kuendelea na safari yake Vienna, Austria, alisema anataka Iran ikubali masharti ya baraza la Umoja wa Mataifa na kurudi kwenye mazungumzo.

Ban Ki Moon anakaa Vienna hadi kesho kwa mkutano na mkuu wa shirika la IAEA, Mohammed El Baradei.

Katibu mkuu huyu pia aliomba jumuiya ya kimataifa kumuunga mkono mwakilishi maalum ya Umoja wa Mataifa katika suala la Kosovo, Martthi Ahtissari, ambaye siku hizi anaongoza mazungumzo kati ya wapatanishi wa Serbia na Kosovo juu ya mustakabali wa eneo la Kosovo. Suala hilo ni mada ambapo mawaziri wa Ujerumani na Urusi, Steinmeier na Lawrow, hawakukubali kwenye mkutano wao wa leo mjini Berlin. Lawrow alisema haitaki suluhisho la kulazimishwa kwa Kosovo akimaanisha Kosovo kupewa uhuru. Waziri Steinmeier alijibu kwa njia ya kidiplomasia lakini alikiri kuwa kuna misamamo tofauti kuhusu suala hilo.