1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaahidi kuibana Korea Kaskazini hadi izungumze

Iddi Ssessanga
27 Aprili 2017

Marekani imeahidi kuongeza mbinyo dhidi ya Korea Kaskazini, kuilaazmisha kurejea kwenye meza ya mazunguzo kuhusiana na programu yake ya nyuklia, lakini ilisema hailengi kuuangusha utawala wa Kim Jong-Un.

https://p.dw.com/p/2bzGT
USA Donald Trump und Mike Pence
Rais Donald Trump na makamu wake Mike Pence wakiondoka kwenye mkutano wa maelezo kwa bunge la Seneti kuhusu Korea Kaskazini, katika ikulu ya White House, Aprili 26,2017.Picha: Reuters/K. Lamarque

Msimamo huo wa Marekani, ambao ulionekana kuashiria utayarifu wa kumaliza njia zote zisizo za kijeshi licha ya onyo za mara kwa mara kwamba njia zote zinazingatiwa, umekuja katika taarifa kufuatia mkutano usiyo wa kawaida katika ikulu ya Marekani - White House uliowahusisha wajumbe wote wa baraza la seneti.

Taarifa iliotolewa na waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson, waziri wa ulinzi Jim Mattis na Mkurugenzi wa idara ya Intelijensia Dan Coats, iliielezea Korea Kaskazini kama kitisho kikubwa cha usalama wa taifa na kipaumbele cha sera ya kigeni.

Democrats na Republican waafiki mkakati wa serikali

Mmoja wa maseneta waliohudhuria mkutano wa ikulu Chris Coons kutoka chamacha Democrat, alisema wabunge hawakupatiwa maelezo kuhusu njia makhsusi za kijeshi au kuombwa kuidhinisha shambulili, lakini aliwaambia waandishi habari kuwa malezo waliopewa yalikuwa ya busara.

Nordkorea Machthaber Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un akisimamia ufyatuaji wa makombora manne ya masafa marefu na jeshi la Korea Kaskazini (KPA), wakati wa luteka za kijeshi katika eneo ambalo halikutajwa nchini Korea Kaskazini, Machi 7,2017.Picha: Getty Images/AFP

"Nimetiwa moyo kwamba waliamua kulitolea maelezo baraza zima la Seneti. Yalikuwa maelezo yenye busara ambamo ilibainika wazi ni mawazo kiasi gani na maandalizi yanafanywa kuandaa mikkakati ya kijeshi ikiwa itahitajika, na mkakati wa kidiplomasia unaonivutia kwa kueleweka vizuri na wenye kulingana na kitisho chenyewe," alisema seneta Coons kutoka jimbo la Delaware.

Kitisho cha nyuklia na makombora kutoka Korea Kaskazini, kinaelezwa kuwa changamoto nzito zaidi ya kiusalama inayoukabili utawala wa rais Donald Trump kwa wakati huu. Trump ameahidi kuizuwia Korea Kaskazini kuwa na uwezo wa kuishambulia Marekani kwa kutumia kombora na nyuklia, uwezo ambao watalaamu wanasema inaweza kuupata baada ya mwaka 2020.

Tarifa ya maafisa hao wa juu wa serikali ilisema mkakati wa rais unalenga kuishinikiza Korea Kaskazini kuvunja programu zake za utengenezaji na uenezaji wa nyuklia na makombora ya masafa marefu na ya kati, kwa kuimarisha vikwazo vya kiuchumi na kuchukuwa hatua za kidiplomasia pamja na washirika wake.

Korea Kaskazini yakejeli vitisho vya Marekani

Awali wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini ilizitaja juhudi za Marekani kujaribu kuilaazimisha Pyongyang kuachana na silaha zake za nyuklia kupitia vitisho vya kijeshi na vikwazo, kuwa ndoto za kufikirikik, na kuzifananisha juhudi hizo na kufagia bahari kwa kutumia ufagio.

Nordkorea provoziert mit weiterem Raketentest
Korea Kaskazini ikionyesha uwezo wake wa makombora wakati wa maadhimisho ya miaka 105 ya kuzaliwa kwa kiongozi wa zamani wa taifa hilo Kim Il-Sung mjini Pyongyang, Aprili 15,2017.Picha: Gettty Images/AFP/E. Jones

Uamuzi wa kuchukuwa hatua isiyo ya kawaida ya kuzungumza na maseneta katika viwanja ya ikulu, badala ya bungeni, ulisanifiwa kutilia mkazo ukubwa wa kitisho hicho, alisema afisa mwandamizi wa usalama wa taifa ambaye hakutaka kutaja jina lake. Korea Kaskazini imeapa kuishambulia Marekani na washirika wake barani Asia, pale itakapoona ishara ya mwanzo tu ya shambulio lolote kwenye ardhi yake.

Katika hatua ya kuonyesha nguvu, Marekani imetuma meli kubwa ya kubeba ndege ya USS Carl Vinson karibu na rasi ya Korea, ambako itaungana na USS Michigan, ambayo ni nyambizi ya nyuklia iliotia nanga Korea Kusini siku ya Jumanne. Jeshi la majini la Korea Kusini limesema litafanya luteka za kijeshi pamoja na kundi la mashambulizi la Marekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae,afpe

Mhariri: Zainab Aziz