1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaanzisha hatua zisizo kifani kukomesha mgogoro wa kifedha

Mohamed Dahman20 Septemba 2008

Serikali ya Marekani imeanzisha kile Rais George W. Bush alichokiita hatua zisizokifani kukomesha mgogoro mbaya kabisa wa kifedha kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miongo kadhaa.

https://p.dw.com/p/FLod
Rais George W. Bush wa Marekani.Picha: AP

Bush ameuambia mkutano wa waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani kwamba ununuzi wa mikopo mibaya kutoka mabenki ni wakati muhimu sana katika historia ya uchumi wa Marekani.

Bush anasema matatizo ambayo yalianzia katika masoko ya mikopo na kwanza kujitokeza katika fani ya mikopo ya nyumba imezagaa kwenye mfumo wao mzima wa fedha kulikokuja kusababisha kumomonyoka kwa imani ambako kumepelekea kusita kwa mabadilishano mengi ya fedha ikiwa ni pamoja na mikopo kwa walaji na wafanyabiashara wanaotaka kuongeza na kuanzisha ajira.

Anasema kama matokeo lazima wachukuwe hatua hivi sasa kulinda afya ya uchumi wao kutoka na hatari kubwa inayoukabili.

Hapo jana waziri wa fedha wa Marekani Henry Paulson ametangaza mpango wa kununuwa mali zenye matatizo kutoka mashirika ya fedha ambayo yeye na mwenyekiti wa benki kuu ya Marekani Ben Bernanke wamesema unaweza kugharimu hadi dola trilioni moja.

Wakati huo huo hakimu wa masuala ya kufilisika mjini New York ameidhinisha mpango wa benki ya uwekezaji ya Lehman Brothers ya Marekani kuuza uwekezaji wake na biashara zake kwa benki ya Barclays ya Uingereza.