1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaapa kuwateketeza Wanamgambo wa IS

10 Septemba 2014

Waziri wa nje wa Marekani John Kerry yuko ziarani mjini Baghdad kuhimiza juhudi za kuunda muungano dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa dola ya kiislam-IS ,huku rais Obama akitarajiwa kutangaza mkakati maalum Leo usiku

https://p.dw.com/p/1D9iz
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters/Brendan Smialowsky

Juhudi za kimataifa kukabiliana na kitisho kinachozidi kuongezeka cha wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam IS zimeshika kasi.

Nchini Iraq kwenyewe Marekani inaendelea na kampeni yake ya kuhujumu vituo vya IS kaskazini ya Iraq na kwa namna hiyo kuwasaidia pakubwa wanajeshi wa serikali na wakurd waliofanikiwa kuyakomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na wafuasi hao wa itikadi kali tangu juni tisa iliyopita.

Miezi miwili na nusu baada ya ziara yake ya kwanza mjini Baghdad kuwahimiza wairaq waunde haraka serikali itakayojumuisha jamii zote ili kuweza kukabiliana na wanamgambo wa IS,waziri Kerry aliyewasili hivi unde mjini Baghdad anatazamiwa kuelezea uungaji mkono wake kwa serikali mpya inayoongozwa na waziri mkuu Haidar al-Abadi.Wakati wa mazungumzo yake pamoja na viongozi wa Iraq,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atashadidia kuhusu jukumu la Iraq katika kuunda "Ushirika wa dunia" ili kuwashinda nguvu wanamgambo wa IS.

Baada ya Baghdad waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atakwenda Jeddah kuonana na mawaziri wenzake kutoka mataifa sita ya kifalme ya Ghuba wanaotaka wapatiwe ufafanuzi kabla ya kujiunga na ushirika huo wa kimataifa ulioanzishwa na Marekani.

Rais Obama kufafanua Mkakati dhidi ya IS

Marekani imezidisha kasi ya juhudi zake katika mkutano wa jumuia ya kujihami ya NATO ambapo mataifa kadhaa yameelezea utayarifu wa kujiunga na ushirika huo.

IS Kämpfer
Wanamgambo wa itikadi kali wa dola ya kiislam ISPicha: picture alliance/dpa

Baada ya kusita sita,rais Barack Obama anatarajiwa kuelezea mkakati wa Marekani wa "kuwadhoofisha na baadae kuwateketeza wanamgambo wa IS,atakapolihutubia taifa kwa njia ya televisheni leo usiku.

"Nnataka wamarekani waelewe kitisho kilichoko na waamini tunaweza kukabiliana nacho" alisema rais Obama jumapili iliyopita akiahidi mashambulio makali zaidi bila ya kupelekwa lakini wanajeshi wa nchi kavu nchini Iraq.

Rais Obama hatazamiwi kutangaza ratiba ya opereshini hizo za kijeshi,hata hivyo ikulu ya Marekani imeshasema hazitakuwa za muda mfupi.

Na jee opereshini zitaenea hadi Syria?

Jana rais Obama alikutana na viongozi wa baraza la Congress,akijiandaa kwa hotuba atakayoitoa leo usiku.Kabla ya hapo alisema ana uwezo wa kupitisha maamuzi muhimu ya kupanua opereshini za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa IS hata bila ya kuomba ruhusa ya baraza la Congress.

Barack Obama / IS / USA
Rais Barack Obama akihutubia Agosti 20 mwaka huu kuhusu azma ya Marekani ya kuwaandama wanamgambo wa ISPicha: Reuters

Katika wakati ambapo rais Obama anajiandaa kwa opereshini kali dhidi ya IS kaskazinmi mwa Iraq,kuna wanaojiuliza kama katika hotuba yake leo usiku atazungumzia pia kuhusu kupanuliwa opereshini hizo hadi Syria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga