1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege isiyokuwa na rubani

6 Agosti 2015

Marekani imefanya shambulizi lake la kwanza kutokea nchini Uturuki dhidi ya ngome ya Dola la Kiislamu nchini Syria. Hayo ni wakati Uturuki ikiapa kuwa tayari vita vyake yenyewe dhidi ya wanamgambo hao wa itikadi kali.

https://p.dw.com/p/1GBBq
Ndege ya Uturuki ikifanya mashambulizi
Ndege ya Uturuki ikifanya mashambuliziPicha: Reuters/M. Sezer

Afisa mmoja wa Uturuki ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ndege ya Marekani isiyoruka na rubani ilifanya shambulizi moja la kutokea angani nchini Syria karibu na Raqa, mji wa kaskazini mwa Syria ambao kundi la IS linauona kuwa ngome yake kuu. Ndege hiyo iliruka kutoka kambi ya jeshi la angani ya kusini mwa Uturuki, Incirlik, ambayo serikali ya Uturuki sasa imeliruhusu jeshi la Marekani kuitumia kwa mashambulizi dhidi ya maeneo ya IS nchini Syria.

Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje Mevlut Cavusoglu alitangaza kuwa Uturuki iko tayari kuanza “vita vikamilifu” dhidi ya IS nchini Syria pamoja na Marekani, baada ya miezi kadhaa ya kusalia kando ya kampeni inayofanywa na jeshi la muungano linaloongozwa na Marekani. Wizara ya ulinzi ya Marekani ilitangaza wiki hii kuwa ndege za Marekani zisizoruka na rubani ziliondoka katika kambi ya Incirlik ili kufanya safari za uchunguzi kaskazini mwa Syria, lakini hii ndio mara ya kwanza ambapo shambulizi limefanywa.

Uturuki yakosolewa

Uturuki, ambayo kwa muda mrefu imekosolewa kwa kushindwa kuwazuia wanamgambo kuingia na kutoka kupitia mipaka yake na Syria, kufikia sasa imefanya kampeni ya wiki mbili ya “kupambana na ugaidi” kwa kuwalipua kwa mabomu na makombora wanamgambo wa Kikurdi. Lakini Cavusoglu ameashiria baada ya mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry nchini Malaysia kuwan Uturuki itaimarisha kampeni yake dhidi ya wapiganaji hao wa jihadi.

Selahattin Demirtas, mwenyekiti wa chama cha HDP
Selahattin Demirtas, mwenyekiti wa chama cha HDPPicha: Reuters/U. Bektas

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wiki iliyopita alisema kuwa kuundwa kwa maeneo salama ndani ya Syria, yasiyokuwa na vitisho vyovyote, kutasaidia kuwarejesha nyumbani karibu wakimbizi milioni 1.8 wanaohifadhiwa nchini Uturuki.

Uturuki sasa inapanga kuunda muungano mdogo utakaozijumuisha nchi za Saudi Arabia, Qatar na Jordan, washirika wa NATO Uingereza na Ufaransa pamoja na Marekani katika kupigana na kundi la IS ambalo liliorodheshwa kuwa la kigaidi mwaka wa 2013.

Wapiganaji wawili wauwawa

Kwingineko, wapiganaji wawili wa jihadi wanaozungumza Kijerumani wanaodai kuwa wafuasi wa kundi la IS wametishia kufanya mashambulizi Ujerumani. Mkanda wa video uliowekwa kwenye internet unawaonyesha wanaume hao wakitumia bunduki zao kuwauwa mateka wawili waliopiga magoti na kufungwa mikono katika mji wa kale wa Syria, Palmyra, ambao SI iliukamata mwezi Mei.

Mmoja wa washukiwa mikonono mwa polisi
Mmoja wa washukiwa mikonono mwa polisiPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

Mmoja wa wanaume hao anaonekana akimtishia Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akiapa kulipiza kisasi “damu ya waislamu iliyomwagika nchini Afghanistan“ ambaki Ujerumani ilituma majeshi kama sehemu ya jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO, na msaada wao kwa jeshi la muungano linalopambana na IS.

Shirika la ujasusi la Ujerumani linakadiria kuwa Wajerumani 600 wamejiunga na makundi ya jihadi nchini Syria na Iraq.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo