1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yafuatilia makundi ya Kigaidi

14 Juni 2012

Marekani imeanzisha mtandao wa siri wa jeshi la anga katika bara la Afrika kuchunguza mwenendo wa kundi la Al-Qaeda na makundi mengine ya kigaidi ikiwa ni nia ya Rais Obama ya kurejesha hali ya amani barani humo.

https://p.dw.com/p/15ERe
Rais Obama- Camp David
Rais Obama- Camp DavidPicha: dapd

Kulingana na ripoti katika gazeti la Washington Post la nchini Marekani kumekuwa na safari za ndege ndogo zisizokuwa na rubani zikitokea katika vituo vya kijeshi vya taifa hilo na kutua katika misitu ya mataifa ya bara la Afrika na kuzunguka katika ukanda huo kufuatilia nyendo za makundi ya kigaidi.

Marais Barack Obama na Francois Hollande
Marais Barack Obama na Francois HollandePicha: AP

Vita vya ugaidi kwa muongo mmoja

Ufuatiliaji wa makundi hayo ya kigaidi ulianza mwaka 2007 katika vita dhidi ya ugaidi vilivyoanza muongo uliopita. Vituo vya kijeshi vilivyopo Burkina Faso na Mauritania vinatumika ipasavyo kuwasaka wanamgambo wa Al-Qaeda waliopo katika eneo la Maghreb na kituo cha Kijeshi kilichopo Uganda kinatumika kuwasaka wanamgambo wa Lords Resistance Army wanaongozwa na Josephy Kony.

Kumekuwa na mpango wa kuazishwa kituo cha kijeshi Sudan Kusini kwa nia kumsaka Kony. Huku katika ukanda wa Afrika ya Mashariki ndege za kijeshi za Marekani zimeonekana kuzunguka katika mataifa ya Djibout, Ethiopia, Kenya na visiwa vya ushelsheli kufuatilia nyendo za Al-Shabab.

Miongoni mwa kambi za kivita za siri, ipo katika mji wa Quagadougou katika taifa lenye waislamu wengi la Burkina Faso huko Afrika ya Magharibi. japokuwa serikali ya taifa hilo kila inapoulizwa inakataa kukiri kama kuna kambi hiyo ya kivita .

Mpango mkakati wa Marekani

Sambamba na hilo Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kuja na mpango wa mkakati wa kukuza biashara, Usalama na demokrasia barani Afrika nia kubwa ni kukuza uchumi wa bara hilo.

Mkakati huo unatazamwa kama nia ya rais wa Marekani kulisadia bara la Afrika ili kuweza kusonga mbele kimaedeleo kutokana. Inatazamwa kuwa mpango mkakati huo wa Rais Obama utakuwa na nafasi kubwa kupambana na njaa, ukame na hali ya kukosekana kwa amani ambapo bara la Afrika kwa muda mrefu linakumbwa na migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na sasa matatizo ya ugaidi.

Rais Obama mpaka sasa amewaalika viongozi wa Afrika kutoka mataifa ya Benin, Ethiopia, Ghana na Tanzania katika mkutano wa G8 huko Camp David. Huku kukiwa na changamoto kubwa kwa China kuvutiwa mno na uwekezaji katika bara hilo.

Kwani mpaka sasa China imewekeza zaidi ya Uro bilioni 120 ambapo muongo mmoja uliopita ilikuwa na uwekezaji wa uro bilioni 20 tu.

Rais Obama akiwa Ghana

Akiwa nchni Ghana Julai 2009 Rais Obama alisema "Ni heshima kubwa kwangu mimi leo hii kuzungumza katika Bunge la Ghana na ninashukuru kwa kunipokea vizuri mimi na familia yangu hapa."

Septemba 11-World Trade Center
Septemba 11-World Trade CenterPicha: AP

Rais Obama anaongeza kuwa ni kweli bara la Afrika linahitaji uwekezaji mkubwa lakini matumaini mazuri yajayo kwa bara hilo yako mikononi mwa Waafrika wenyewe.

Mwandishi:Adeladius Makwega/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu